Habari za michezo

JKT, STEIN WARRIORS KAZI IPO UFUNGUZI BDL

Vardo May 13, 2026 8:31 am

ILE Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), inarudi na tayari timu shiriki 16 zinajifua kwa ajili ya kipute hicho kinachotarajiwa kuanza siku nne zijazo, ambapo kamishna wa Ufundi na Mashindano, Shabani Mahobonya amesema ufunguzi unafanyika Mei 17 kwa mchezo kati ya Stein Warriors na JKT.

Mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 2:00 usiku katika Uwanja wa Donbosco, Oysterbay, utatanguliwa na mechi kati ya Ukonga Kings na Mlimani BC na baadaye Tausi Royals itacheza dhidi ya Vijana Queens katika gemu nyingine ya Ligi ya Kikapu kwa Wanawake Dar es Salaam (WBDL).

“Ligi ya kikapu ya BDL rasmi itaanza Mei 16 katika uwanja wa Donbosco Upanga, lakini tumepanga ufunguzi ufanyike Mei 17 (Jumapili),” amesema Mahobonya akitaja michezo itakayochezwa Jumamosi, wiki hii kuwa ni kati ya Ukonga Queens na Mgulani Queens, City Queens dhidi ya Kurasini Divas, UDSM Queens na Pazi Queens upande wa wanawake.

Michezo mingine ni Chui dhidi ya Srelio, Twalipo Queens itakabiliana na Polisi Stars, Mchenga BC itaumana na Magone BC, ilhali DB Troncatti itakipiga na Jeshi Stars huku Savio ikiwasha dhidi ya Vijana.

Mchezo kati ya JKT na Stein Warriors unaojulikana kama Dabi ya BDL umepewa jina hilo kutokana na ushindani mkubwa uliopo kati ya timu hizo na mara ya mwisho timu hizo zilipokutana ilikuwa mwaka jana, ambapo JKT ilipewa ushindi baada ya mwamuzi wa mchezo kuvunja pambano.

Katika mechi hiyo ilikuwa hivi; kamisaa wa mchezo, Mussa Kango alimwamuru kocha wa Stein Warriors, Karabani Karabani atoke katika benchi kutokana na kuchelewa kwa dakika 15, jambo lililosababisha mwamuzi kuvunja pambano. Kabla ya mwamuzi kuvunja pambano katika robo ya nne, Stein Warriors ilikuwa inaongoza kwa pointi 41-33.

Akizungumzia mchezo kati ya timu hizo, mmoja wa mashabiki wa kikapu, Salumu Issa aliitabiria Warriors kufanya mambo makubwa mwaka huu, akisema: “Nachosema katika ligi ya BDL, mpinzani wetu ni Dar City siyo timu nyingine.”

Stein Warriors inajivunia nyota wawili wa kimataifa waliosajiliwa kutoka DRC Congo ambao ni Daniel Kola na Moise Bukengu, ambapo mwaka jana, Bukengu akiwa na Savio alikuwa mfungaji bora wa ligi akitupia pointi 351 na kumuacha kwa mbali aliyeshika nafasi ya pili, Isaya William wa DB Oratory aliyetupia alama 235.

Wachezaji wengine waliosajiliwa na timu hiyo ni Jimmy Brown, Tyrone Adrew, Swalehe Burhan, Ally Mohamed, Gwakisa Mwakafwisya, Adam Kassim, Mwinyipembe Jumbe, David Mshamu, Mwalimu Kijogoo, Brian Mramba, Faraji Juma, Abasi Kiango na Spoican Ngoma.

Kwa upande wa JKT, kikosi kitakuwa na Omary Ndula, Jacob Mganga, John Rogath, Rajabu Mbonde, Prudensius Shija, Mussa Chacha, Klaus Mshamu, Elias Paul, George Peter, January Wilbard, Daudi Songo, Anthony Gosbert, Ndalawa Juma, Dotto Zepania, Sidy Shabani na Ezra Elias wanaofundishwa na kocha Christiana Mwakingili.

DAR CITY KUKIWASHA JUNI 12 BDL

Mahobonya amesema Dar City itaanza kampeni ya kutetea ubingwa Juni 12 katika Uwanja wa Donbosco na kwamba imepangiwa tarehe hiyo kutokana na kupewa mapumziko baada ya kurejea kutoka katika mashindano ya mchujo (playoff), kuwania kufuzu robo fainali za Ligi ya Kikapu Afrika (BAL).

“Sisi kama BDL tunayaheshimu sana mashindano hayo, kwani (Dar City) imetuheshimisha Mkoa wa Dar es Salaam na taifa kwa ujumla,” amesema Mahobonya.

Timu hiyo imeweka kambi ya maandalizi ya mashindano hayo huko Dubai, ikitarajia kuanza Mei 22 hadi 31 nchini Rwanda, ambapo inazikutanisha timu nne zilizofuzu katika kundi la Kalahari Conference na nne za kundi la Sahara Conference.

Dar City itacheza dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, Al Ahly (Misri) dhidi ya Ville de Dakar (Senegal), Club African (Tunisia) dhidi ya Al Ahly (Libya), huku RSSB Tigers (Rwanda) ikicheza dhidi ya FUS Rabat (Morocco).

Akiizungumzia timu hiyo, kocha wa kikapu  Kassim Juma amesema maandalizi bora yatawaongezea chachu wachezaji kufanya vizuri katika hatua  ya robo fainali ambayo itaipaisha zaidi katika mchezo huo Afrika na duniani kwa ujumla.

REEL DREAM KUZIVURUGIA KONGWE?

Baada ya Reel Dream kushika nafasi ya 10 katika Ligi ya Kikapu kwa Wanawake Dar es Salaam (WBDL), mwaka jana, kiongozi wa timu hiyo, Emmanuel Mkono, amesema msimu huu wanatarajia kuwashangaza mashabiki wengi wa mchezo huo.

Mkono ameliambia Mwanaspoti kuwa walianza mikakati ya kuimarisha kikosi baada ya ligi hiyo kumalizika mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji nyota wa kimataifa na wazawa.

Aliwataja wachezaji wa kimataifa kuwa ni Mzimbabwe Dorcas Marondera na Waganda Ruth Atuheira na Evelyne Nakiying.

Wachezaji wazawa waliosajiliwa ni Judith Nyari, Husna Mwegelo, Rebecca Steven, Shadya Maginga, Lightness Sausi, Glory Njau, Magreth Mwafulila, Maria Boniventure, Ratifa Mwembe, Rahma Simba, Happiness Danford, Tusekile Kajigili, Hafsa Salim, Tumpale Mwatembe na Neema Mathew.

Timu hiyo itakuwa chini ya makocha Deogratus Flame na Alex Bwana na kwa mujibu wa Mkono, walipata wazo la kuianzisha baada ya kuona timu za wanawake hazipati sapoti kubwa kutoka kwa wadau wa mchezo huo.

“Kwa uwezo wangu nimeona niwape sapoti (wanawake) na kuwapa thamani kwenye mchezo huu,” amesema Mkono. Timu ya Reel Dream itaanza kampeni ya kuwania ubingwa msimu huu Mei 20 itakapocheza na Vijana Queens katika Uwanja wa Donbosco.

MUDA WA KUCHEZA NA KUSHINDA KWA MICHEZO YA KISASA YA KASINO MBEYA CITY, COASTAL LEO NI PRESHA NA HESABU KALI