HESABU za kukwepa aibu ya kushuka daraja inaendelea kuzipa presha timu za Ligi Kuu Bara, huku Kocha wa Mbeya City, Saluma Mayanga na Fikiri Elias wa Coastal wakivimbiana kusaka pointi tatu kujiweka pazuri.
Timu hizo ambazo zinatarajia kukutana leo Jumatano katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kila upande unahitaji ushindi ili kujinasua nafasi nne za hatari ya kushuka daraja.
Hadi sasa Coastal Union ipo nafasi ya 13 kwa pointi 22, huku wenyeji Mbeya City wakiwa nafasi ya 14 kwa pointi 21 baada ya timu hizo kucheza mechi 22 na kufanya mchezo huo kuwa wa jasho na damu kujiweka pazuri.
Hata hivyo, timu hizo zinakutana ikiwa Coastal Union haijapata ushindi kwenye michezo miwili mfululizo ikiruhusu mabao sita ikianza kufungwa 3-2 dhidi ya Fountain Gate kisha kulala 3-0 mbele ya vinara wa ligi hiyo, Yanga.
Kwa upande wa Mbeya City utakuwa mchezo wa nne kwa Mayanga, ambapo ameshinda mmoja sawa na sare na kichapo alichopokea.
Mayanga alisema wanafahamu ugumu wa mchezo huo, lakini kutokana na hali waliyopo hawana sababu za kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanashinda ili kuweka matumaini mapya kikosini.
“Tunajua tunakutana na wapinzani wagumu kwenye ligi na wote hatujaachana sana, tunajua umuhimu wa pointi tatu katika kufufua matumaini ya kujiweka pazuri na pengine kukwepa kushuka daraja.
“Baada ya kupoteza mchezo uliopita tumefanyia kazi makosa na matarajio yangu vijana wangu watafanya kazi nzuri kuhakikisha hatupotezi pointi yoyote kesho (leo), mashabiki waje kwa wingi kutusapoti,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wake Kocha Elias alisema mchezo huo ni muhimu sana kwao katika hesabu za kubaki salama Ligi Kuu akieleza kuwa nyota wa kikosi hicho wako tayari kwa dakika 90 kuhakikisha wanashinda.
“Tunaenda uwanjani kwa lengo la pointi tatu, mchezo huu ni mbinu na hesabu kali za pointi tatu, naamini vijana wangu watafanya kazi na kuipa ushindi timu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo,” alisema kocha huyo.