Habari za michezo

MTIBWA SUGAR YAPIGA HESABU ZA KUSALIA LIGI KUU

Vardo May 13, 2026 8:52 am

PAMOJA na kukubali ugumu wa namba kikosini, Straika wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh amesema bado ni mapema kuitabiria timu hiyo magumu Ligi Kuu Bara msimu huu kwani mechi nane zilizobaki zinaweza kuamua lolote.

Alisisitiza kuwa, Mtibwa Sugar kushuka daraja ni ndoto kwani uwezo wa mchezaji mmoja mmoja uwanjani unaweza kuamua hatma ya timu akieleza kuwa kwa sasa kila mchezo kwao ni fainali nzito ya pointi tatu.

Nyota huyo aliyeirejesha timu hiyo Ligi Kuu kwa kuongoza orodha ya wafungaji bora msimu uliopita kwa mabao 22 katika Ligi ya Championship, hajawa na wakati mzuri kikosini akikumbana na ushindani wa namba.

Mtibwa Sugar iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo mwaka 1999 na 2000, imerejea msimu huu baada ya kudumu Ligi ya Championship msimu mmoja na kwa sasa haina matokeo mazuri kwenye mashindano hayo.

Timu hiyo iliyocheza mechi 22, imekusanya pointi 23 na kuwa nafasi ya 12, matokeo ambayo yanaipa presha katika vita ya kukwepa kushuka daraja msimu huu kufuatia ushindani uliopo Ligi Kuu.

Nyota huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa, licha ya vita nzito iliyopo na ugumu kwenye ligi, lakini Mtibwa Sugar bado ina nafasi kubwa ya kubaki salama kutokana na ubora wa timu kwa mchezaji mmoja mmoja.

Alisema kwa sasa wanaendelea na mipango ya kuzicheza vizuri mechi nane zilizobaki wakianza na mchezo ujao dhidi ya KMC, Mei 14 mwaka huu kuhakikisha wanashinda na kupanda nafasi za juu.

“Bado tunao uwezo wa kubadili upepo, kiujumla ugumu na ushindani ni mkali kwa sababu kila timu inaonesha upinzani lakini naamini kwa ubora wa kikosi chetu hatuwezi kurudi Championship,” alisema.

Straika huyo ameongeza kuwa, ishu ya ugumu wa namba kikosini ni kutokana na uamuzi wa kocha kutegemeana na mipango ya mchezo husika, akibainisha kuwa hata ubora wa wachezaji ni sababu nyingine.

“Uamuzi wa nani aanze au kusubiri ni wa kocha, hii inaonesha namna timu ilivyo na kikosi kipana chenye uwezo, kimsingi naamini muda wangu ukifika nitacheza zaidi ila nachoomba ni timu ipate ushindi,” alisema nyota huyo mwenye bao moja Ligi Kuu Bara.

MBEYA CITY, COASTAL LEO NI PRESHA NA HESABU KALI KAGOMA AFURAHI KURUDI KIGOMA, AITAMANI DAKIKA 90 DHIDI YA MASHUJAA