Habari za michezo
KAGOMA AFURAHI KURUDI KIGOMA, AITAMANI DAKIKA 90 DHIDI YA MASHUJAA
Vardo
May 13, 2026
8:57 am
KIUNGO mkabaji wa Simba SC, Kagoma, amesema ana hamasa kubwa ya kurejea kucheza mkoani Kigoma huku akiweka wazi kuwa ni jambo maalum kwake kurudi nyumbani akiwa sehemu ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Kigoma amesema safari ya kuelekea Kigoma kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC imeibua hisia tofauti kwake kutokana na kucheza mbele ya mashabiki wa nyumbani akiwa na jezi ya Simba.
Nyota huyo amesema kurejea Kigoma si jambo la kawaida kwake kwani ni sehemu aliyokulia na kuanza safari yake ya soka kabla ya kupata nafasi ya kucheza katika kiwango cha juu zaidi nchini.
Kiungo huyo ameweka wazi kuwa anatamani kupata nafasi ya kucheza katika mchezo huo wa Alhamisi ili aweze kuonyesha uwezo wake mbele ya watu wa nyumbani wanaoendelea kumuunga mkono.
“Ni furaha kubwa kurudi nyumbani Kigoma nikiwa mchezaji wa Simba. Nikipata nafasi ya kucheza itakuwa jambo la kipekee sana kwangu,” amesema Kagoma.
Mbali na furaha hiyo, Kagoma amesema Simba ipo Kigoma kwa malengo makubwa ya kuhakikisha wanapata ushindi muhimu dhidi ya Mashujaa FC katika mbio za kusaka mafanikio msimu huu.
Simba itashuka dimbani Mei 14 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, huku mashabiki wengi wakitarajiwa kujitokeza kushuhudia mchezo huo wenye ushindani mkubwa.