KIUNGO wa KMC, Omary Chibada amesema amekuwa akivutiwa na kiwango cha Duke Abuya kutokana na namna anavyocheza kwa utulivu mkubwa.
Abuya alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025 akitokea Ihefu ambayo sasa inaitwa Singida Black Stars, tangu hapo amekuwa kiungo mahiri ndani ya kikosi hicho.
Chibada alisema moja ya vitu vinavyomfanya amkubali Abuya ni nidhamu yake ya kucheza pamoja na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi akiwa kwenye mazingira yenye presha kubwa ya mchezo.
Alieleza kuwa, Abuya ni miongoni mwa viungo ambao wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na kujituma kwake kila anapopewa nafasi ya kucheza.
“Duke ni mchezaji mzuri sana, anacheza kwa utulivu mkubwa na ana nidhamu ya hali ya juu uwanjani. Hivyo ni vitu vinavyomfanya kuwa tofauti,” alisema Chibada.
Kiungo huyo raia wa Kenya, amekuwa mmoja wa wachezaji wanaoaminika ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na uwezo wake wa kutuliza mchezo na kusaidia timu kumiliki mpira kwa muda mrefu.
Mbali na kumzungumzia Abuya, Chibada aliyewahi kuichezea Yanga na Mbeya City kabla ya Januari 2026 kutua KMC, alisema ushindani wa Ligi Kuu Bara msimu huu umekuwa mkubwa akieleza kuwa timu nyingi zimejipanga vizuri tofauti na ilivyokuwa zamani.
Alisema hivi sasa kila timu inapambana kupata matokeo mazuri jambo ambalo limeongeza ugumu wa mechi nyingi kwenye ligi hiyo.
“Kwa sasa hakuna mechi rahisi kwa sababu timu nyingi zimejipanga vizuri. Ushindani umeongezeka sana na kila timu inapambana kuhakikisha inapata matokeo bora,” alisema Chibada.
Chibada aliyecheza mechi sita za Ligi Kuu Bara akiwa KMC, kikosi hicho kina kazi ya kufanya msimu huu kuepuka kushuka daraja kwani hivi sasa kinashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo kikikusanya pointi tisa, zikibaki mechi nane.