Habari za michezo
SERENGETI BOYS MZIGONI IKISAKA TIKETI KOMBE LA DUNIA
Vardo
May 14, 2026
10:07 am
ILE siku ambayo Watanzania wengi walikuwa wakiisubiri imewadia, ambapo timu ya Taifa ya soka chini ya miaka miaka 17 (Serengeti Boys), leo inaanza safari yake katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika U17 kucheza dhidi ya Msumbiji, mechi itakayopigwa Uwanja wa Mohammed VI Football Academy (pitch 11 Sale) nchini Morocco.
Kwenye michuano hiyo iliyoanza jana Jumatano, Mei 13, 2026 nchini Morocco na kutarajiwa kumalizika Juni 2, 2026, inashirikisha timu 16, huku Tanzania ikipangwa kundi C na timu za Mali, Angola na Msumbiji. Kumbuka bingwa mtetezi ni Morocco.
Tanzania inaanza hatua ya makundi dhidi ya Msumbiji ambayo haina rekodi nzuri kwenye mashindano hayo kwani hii ni mara ya tatu kushiriki baada ya mwaka 1995 na 2001 ambapo zote iliishia makundi.
Kwa upande wa Tanzania, hii ni mara ya tano kushiriki mashindano hayo baada ya mwaka 2017, 2019, 2021 na 2025, lakini pia haijafanikiwa kuvuka hatua ya makundi.
Hivyo basi, mchezo wa leo kati ya Tanzania na Msumbiji, una historia inayozikutanisha timu mbili ambazo bado zinatafuta mafanikio ya kwanza kwenye soka la vijana Afrika.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu zote kwani kila moja ina ndoto ya kuanza mashindano kwa ushindi ili kujitengenezea nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia U17. Tanzania inaingia ikiwa na morali kubwa baada ya ubingwa wa CECAFA, huku Msumbiji ikiamini inaweza kushinda kutokana na uimara wao wa kiulinzi.
Kwa Tanzania, ushindi wa leo unaweza kuwa hatua muhimu kuelekea kutimiza ndoto ya kihistoria ya kuvuka makundi kwa mara ya kwanza na kupigania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia U17 nchini Qatar kuanzia Novemba 19, 2026 hadi Desemba 13, 2026. Timu kumi kati ya 16 zinazoshiriki michuano hiyo, zitafuzu Kombe la Dunia U17.
Timu nane ambazo zitafuzu moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia U17, ni zile zitakazomaliza nafasi mbili za juu kutoka kila kundi, kisha zingine mbili ili kukamilisha idadi ya timu kumi zitazihusu zilizokuwa na matokeo bora zaidi nafasi ya tatu kwenye makundi yote. Tanzania ilikata tiketi ya AFCON U17 baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya CECAFA iliyofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia.
Ikiwa chini ya Elieneza Nicolaus Nsanganzelu, kikosi hicho kilionyesha uimara mkubwa kuanzia hatua ya makundi ikiwa na kundi B na timu za Uganda, Sudan, Burundi na Djibouti ambapo Tanzania ilimaliza kileleni na pointi tisa.
Moja ya mechi zilizovuta hisia ilikuwa ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Uganda kwenye hatua ya makundi, kabla ya kuwakabili tena wapinzani hao katika mchezo wa fainali. Katika fainali, Tanzania ilionyesha ubora mkubwa dhidi ya Uganda na kushinda kwa mabao 3-2.
Kocha Elieneza alisema: “Mechi yetu na Msumbiji ndio itatoa taswira ya michuano hii na tunakwendaje, tunacheza na Msumbiji ambayo nayo inataka ushindi, kwa hiyo ni mechi ngumu lakini tumejipanga.”