Habari za michezo
EL HADJI DIOUF KUTUMIKIA ADHABU GEREZANI
Vardo
May 15, 2026
5:01 pm
DAKAR, SENEGAL: Nyota wa zamani wa Liverpool, El Hadji Diouf ameamriwa kutumikia hukumu ya kifungo kilichokuwa kimesimamishwa baada ya kushindwa kutoa matunzo ya kila mwezi ya mtoto wake, Keyla.
Diouf ambaye aliichezea Liverpool kati ya 2002 na 2005 alifikishwa mahakamani nchini Senegal mwaka jana na aliyekuwa mkewe Valerie Bishop kwa kushindwa kuhudumia mtoto ambapo aliamriwa kulipa gharama za matunzo.
Lakini, baada ya muda mrefu kupita, wiki hii, Mahakama ya Dakar, imeamuru kifungo cha mwaka mmoja ambacho awali kilisimamishwa kumpa nafasi ya kulipa fedha hizo, pamoja na kuamriwa kulipa Faranga 10 milioni za Afrika Magharibi (sawa na Pauni 13,220).
Valerie, ambaye aliachana na Diouf 2023, alipewa haki ya malezi ya binti yao, Keyla. Na mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool aliagizwa kumlipa Pauni 670 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto, ada za shule na gharama za matibabu.
Sheria za Senegal zina adhabu kuhusu matunzo ya familia, ikiwemo kifungu cha 351 ambacho kinaelekeza adhabu ya kifungo kwa mtu anayekataa kutoa fedha za matunzo.
Mawakili wa Valerie, Baboucar Cisse na Cheikh Sy, walidai kuwa Diouf alikuwa na uwezo wa kifedha kutimiza wajibu wake, lakini aligoma kufanya hivyo. “Diouf ana uwezo mkubwa wa kifedha. Ana uwezo wa kulipa, lakini anakataa kufanya hivyo,” amesema mmoja wa mawakili hao.
Hata hivyo, haijafahamika ni lini ataanza kutumikia kifungo chake na iwapo yupo Senegal au la, kwani mara nyingi amekuwa akiishi ama Uingereza au Ufaransa ambako ana makazi mengine.
Diouf alitumia misimu mitatu akiwa Liverpool, lakini msimu wake wa mwisho aliutumia kwa mkopo katika klabu ya Bolton Wanderers. Hata hivyo, kipindi chake katika klabu hiyo ya Merseyside huenda kilifunikwa zaidi na ugomvi wake na Steven Gerrard.
Florent Sinama-Pongolle, mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, aliwahi kueleza tukio la mzozo kati ya wawili hao wakati wa mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu akisema: “Mapumziko ya kipindi cha kwanza cha mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu kulikuwa na ugomvi kati ya Diouf na Gerrard. Nilipatwa na mshtuko. Unaweza kufikiria vijana wadogo wakiona hili na kuamini kwamba hivyo ndivyo mastaa wa kiwango bora walivyo.
“Wakati wa mapumziko kwenye chumba cha kubadilishia nguo, Stevie G alikuwa akisema, ‘lazima utoe pasi, lazima utoe pasi,’ na Diouf alipandwa na hasira. Hakuwa anazungumza Kiingereza vizuri. Kiingereza chake kilikuwa kibovu. Unajua alifanya nini? Walichukiana sana.
“Steven Gerrard alifika na kumtukana Diouf. Na Diouf hakuweza kujibu, hivyo alimkamata (aliyekuwa kocha wa Liverpool) Gerard Houllier na kusema, ‘mwambie nitamtukania mama yake.’”
Diouf pia aliwahi kuwa na vita vya maneno na gwiji wa Liverpool Jamie Carragher, ambaye aliwahi kusema kuwa alikuwa “mmoja wa washambuliaji wenye wastani mbaya zaidi wa mabao katika historia ya Liverpool” baada ya kushindwa kufunga katika zaidi ya mechi 30.
Carragher ameongeza: “Mbaya zaidi lazima awe El Hadji Diouf. Kwa kweli nilifurahia kucheza dhidi yake kwa sababu ungeweza kumpiga teke, huwezi kuwapiga teke wachezaji wa timu yako mwenyewe.”