BAADA ya kukosa ushindi katika michezo tisa aliyosimamia, hatimaye Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa ameonja pointi tatu za kwanza Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na timu hiyo Februari mwaka huu, huku akianza kuchimba mkwara.
Kabla ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate uliopatikana Mei 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Prisons ilicheza mechi tisa mfululizo bila kupata pointi tatu na kuweka presha kubwa kwa Maafande hao.
Nsajigwa alitua kikosini humo akitokea Transit Camp ya Championship kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Zedekia Otieno raia wa Kenya ambaye alisitishiwa kibarua chake kutokana na matokeo mabovu.
Nyota huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, katika mechi nane ikiwamo ya kombe la Shirikisho la CRDB alizoongoza, aliambulia sare mbili na kupoteza saba na kuiweka Prisons nafasi ya 15 kwa pointi 17 kwenye msimamo wa ligi.
Akizungumza na Soka la Bongo, Nsajigwa mbali na kuwapongeza nyota wake, amesema iwapo wataendeleza kasi hiyo huenda wakaondoka katika nafasi waliyopo na kumaliza salama Ligi Kuu.
Amesema kwa sasa anaendelea kuwaandaa wachezaji kiakili, kisaikolojia na kiufundi kwa mbinu tofauti kuhakikisha mechi saba zilizobaki wanacheza kufa na kupona ili kuinusuru timu kutoshuka daraja.
“Niwapongeze wachezaji kwa kufuata maelekezo na iwapo tutaendeleza kasi na ushindi huu huenda tukaondoka nafasi hii na kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi na pengine kubaki salama,” amesema Nsajigwa.
Kwa upande straika wa timu hiyo George Mpole aliyeipatia bao pekee lililoipa pointi tatu Prisons, amesema matokeo hayo ni sehemu ya malengo yao kwenye michezo inayofuata kuhakikisha wanafanya vizuri.