SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), imesema mchezaji yeyote wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) atakayecheza mashindano ya ndondo, ataadhibiwa kwa kufungiwa michezo mitano ya ligi msimu unaofuata na kutozwa faini ya Sh100,000.
Adhabu hiyo pia imewaangukia waamuzi wanaochezesha ZPL atakayechezesha mashindano hayo atafungiwa kwa michezo mitano na atalipa faini ya Sh200,000.
Taarifa hiyo imetolewa na Ofisa Habari wa ZFF, Mohamed Kabwanga, baada ya tasisi mbalimbali kuwa katika maandalizi ya kuanzisha mashindano ya Ndondo.
Pia, taarifa hiyo ilieleza kuwa kiongozi yeyote wa Ligi Kuu Zanzibar atakayeshiriki katika mashindano hayo atafungiwa kushiriki mechi tano na faini ya Sh300,000.
“Yatakapofanyika hayo kwenye mashindano husika, muandaaji wa mashindano hayo atatozwa faini ya Sh1 milioni sambamba na kufungiwa kuanzisha mashindano hayo kwa miaka miwili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya mashindano ya ZFF sura ya pili kifungu namba nne,” imesema taarifa hiyo.
Vilevile, ZFF imewataka waandaaji wa mashindano hayo kuifuata kanuni ya mashindano ya msimu wa 2025-2026 na 2026-2027 ambayo imetaja mambo mbalimbali ikiwemo masharti ya kuchezesha mashindano hayo pamoja na namna ya kuomba ruhusa kwa maandishi ili kupatiwa kibali.
Pia, ZFF imewataka kutotumia mchezaji yeyote wa Ligi Kuu katika mashindano hayo kwani kuwatumia wachezaji hao sio malengo halisi na hiyo ni kinyume cha kanuni ya shirikisho hilo.
Sambamba na hilo, ZFF imetaka kutochezwa mashindano hayo hadi ligi itakapomalizika na mashindano rasmi ya ZFF kumaliza ikiwemo michezo inayohusisha timu ya Taifa Zanzibar Heroes.
Pia, waandaaji hao wametakiwa kuwasilisha kanuni zao ZFF na kukubaliwa kwa kupitishwa na kamati ya ufundi, kanuni ziwe zinaendana na sheria na utaratibu wa mchezo wa mpira wa miguu.