BAADA ya Hausung FC kupokwa pointi tatu na mabao matatu, ila kocha wa kikosi hicho, Selemani Kitunda Simota ‘Guardiola’ amesema bado hawajakata tamaa ya kupambana ili kukitoa kikosi hicho mkiani, licha ya ushindani mkubwa wa wapinzani wao.
Timu hiyo ilikutana na adhabu ya kupokwa pointi tatu na mabao matatu baada ya kushindwa kusafiri kwa ajili ya mechi ya kikosi hicho dhidi ya Mbeya Kwanza iliyopangwa kufanyika Mei 2, 2026, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini, Tabora.
Pia, Hausung FC ilipigwa faini ya Sh10 milioni, huku mwenyekiti wa timu hiyo, Erasto Haule akifungiwa mwaka mmoja kwa kosa la klabu hiyo kushindwa kabisa kufika uwanjani kwa kuzingatia kanuni ya 31:1 (1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship.
Akizungumza na Soka la Bongo, Kitunda amesema adhabu hiyo imewarudisha nyuma kwa kiwango kikubwa kutokana na nafasi mbaya waliyopo, japo wataendelea kupambana kwa ajili ya mechi sita zilizobakia kwa lengo la kukinusuru kikosi hicho kisishuke.
“Nisingependa kuzungumzia kilichotokea kwa sababu hakiwezi kubadilisha chochote, tumepokea adhabu iliyotolewa na sasa malengo yetu ni kupambania pointi 18 katika mechi zilizobakia, uwezo wa kunusuru timu bado ni mkubwa,” amesema Kitunda.
Kitunda anayefananishwa na Kocha wa Manchester City ya England, Pep Guardiola katika karia yake ya soka amecheza timu mbalimbali za Kikwajuni FC, Polisi Pemba na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo maarufu KMKM FC zote za visiwani, Zanzibar.
Licha ya kucheza Kikwajuni FC, Polisi Pemba na KMKM FC, ila, Kitunda amewahi pia kuzifundisha timu mbalimbali, zikiwemo, Tunduru Korosho, Stand United ‘Chama la Wana’, Cosmopolitan na mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1982, kikosi cha Pan Africans.
Hausung imepanda daraja msimu huu na kushiriki Ligi ya Championship baada ya kuongoza kundi A na pointi 25, ikiungana na mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2024-2025, Gunners FC ya Dodoma, iliyoongoza pia kutoka kundi B na pointi 35.
Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, katika mechi 24, ilizocheza msimu huu imeshinda tatu, sare mbili na kupoteza 19, ikishika nafasi ya 15 na pointi 11, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 15 na kuruhusu 48.