Habari za michezo

BEIMBAYA APATA MATUMAINI MAPYA B19 FC

Vardo May 16, 2026 9:48 am

LICHA ya ushindani uliopo katika Ligi ya Championship hadi sasa, ila Kocha wa B19 FC, Twaha Beimbaya amesema timu hiyo ina nafasi kubwa ya kuepuka kucheza mechi za ‘Play-Off’ ya kushuka daraja, jambo linalowezekana kutimiza malengo hayo.

Akizungumza na Soka la Bongo, Beimbaya amesema licha ya ugeni wa timu hiyo katika Ligi ya Championship ila kuna maendeleo mazuri ya kiuchezaji kwa mchezaji mmoja mmoja, jambo linaloongeza ari ya kupambana katika mechi sita zilizobakia sasa.

“Bado hatupo nafasi nzuri kwa sababu mechi sita ni sawa na pointi 18 ambazo zinaweza kubadilisha mwelekeo wetu wa msimu huu, jambo la muhimu ni kucheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu kila mpinzani ana malengo aliyoweka,” amesema Beimbaya.

Kocha huyo aliyewahi kuifundisha Kiluvya United kwa sasa Barberian, amepewa jukumu la kukiongoza kikosi cha B19 zamani Tanesco kwa mkataba wa miezi sita, baada ya uongozi wa timu hiyo kuachana na Babou Salim kwa makubaliano ya pande mbili.

Beimbaya aliyewahi kuifundisha pia Pan Africans, kwa sasa ameiongoza B19 FC ikishika nafasi ya 12 na pointi 24, baada ya timu hiyo kushinda mechi sita, sare sita na kupoteza 12, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao 22 na kuruhusu 38.

MAABAD AMVAA FEI TOTO WATAALAMU WAONYA KUHUSU JOTO KOMBE LA DUNIA 2026