Habari za michezo
WATAALAMU WAONYA KUHUSU JOTO KOMBE LA DUNIA 2026
Vardo
May 16, 2026
9:53 am
LONDON, UINGEREZA: KUNDI la wataalamu 20 wa kimataifa wa afya, mabadiliko ya tabianchi na sayansi ya michezo wamelionya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwamba hatua zake za sasa za kukabiliana na joto kali kwenye Kombe la Dunia 2026 ni dhaifu na zinaweza kuhatarisha afya na maisha ya wachezaji.
Wataalamu hao wamesema miongozo ya FIFA haizingatii ipasavyo ushahidi wa kisayansi wa sasa na hivyo ni vigumu kuhalalisha uamuzi wa kuendelea na mfumo uliopo wa ulinzi wa wachezaji dhidi ya joto.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashindano yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico yanatarajiwa kukumbwa na viwango vya juu vya joto huku baadhi ya maeneo yakifikia zaidi ya nyuzi 30C hadi 40C wakati wa mchana.
Watafiti wanaonya kuwa viwanja 14 kati ya 16 vinavyotarajiwa kutumika vinaweza kukumbwa na hali hatarishi ya joto kwa wachezaji, hasa pale unyevu na mwanga mkali wa jua vinapounganishwa na joto hilo kali.
FIFA kwa upande wake imesema imejipanga kulinda afya za wachezaji kupitia hatua mbalimbali za usimamizi wa hali ya hewa, ikiwemo ufuatiliaji wa kiwango cha joto na marekebisho ya ratiba pale inapohitajika.
Shirikisho hilo pia limeanzisha mapumziko ya lazima ya dakika tatu kila kipindi kwa ajili ya kupooza mwili wa wachezaji, hatua ambayo itatumika katika kila mchezo bila kujali hali ya hewa.
Aidha, FIFA inatumia kipimo cha Wet Bulb Globe Temperature (WBGT), kinachopima athari ya joto na unyevunyevu kwa mwili, ambapo kiwango cha 28°C kinachukuliwa kuwa hatari kwa wanamichezo wa kiwango cha juu.
Hata hivyo, wataalamu hao wanapendekeza FIFA iongeze muda wa mapumziko ya kupooza mwili hadi angalau dakika sita pamoja na kuahirisha au kusogeza mechi zote zitakazofanyika pale joto litakapozidi kiwango cha 28°C WBGT.
Wataalamu hao wamesema pia vifaa vya kupooza wachezaji viimarishwe zaidi na miongozo ya FIFA iboreshwe mara kwa mara kulingana na tafiti mpya za kisayansi kuhusu athari za joto kali.
FIFA haijatoa majibu ya moja kwa moja kuhusu barua hiyo lakini imesema itaendelea kufuatilia hali ya hewa kwa karibu na kuchukua hatua za dharura kulingana na mazingira ya kila mchezo ili kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa usalama.