Habari za michezo
SIMULIZI VITA YA KUSHUKA DARAJA LA LIGA
Vardo
May 16, 2026
10:03 am
CATALONIA, HISPANIA: Tayari vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Hispania (LaLiga) 2025/26 imeshamalizika. Barcelona wamebeba huku Real Madrid ikiwa na uhakika kumaliza nafasi ya pili na Villarreal na Atletico Madrid zikikamilisha idadi ya timu nne za juu.
Lakini, kuna vita kubwa katika msimamo kwenye timu zinazowania kufuzu Europa na Conference League msimu huu, kwani Real Betis, Celta Vigo, Getafe, Real Sociedad, Athletic Club, Sevilla na Rayo Valecano zote zina nafasi ya kufuzu.
Ukiachana na vita hiyo, kuna vita kubwa kuepuka kushuka daraja. Baada ya siku 143 za mateso na usiku mwingi wa kukosa usingizi, hatimaye kocha Manolo González alipata ahueni japo kwa muda mfupi. Dakika ya 92 ya mchezo wa 19 mwaka huu wa 2026, jambo la ajabu lilitokea, ambapo Espanyol walishinda mechi ya kwanza na mashabiki wao wakalipuka kwa furaha.
Timu hiyo ilikuwa mbele kwa bao moja dhidi ya Athletic Club, lakini kichwa cha kuchelewa cha Gorka Guruzeta kilitikisa zaidi mioyo yao kuliko mwamba wa goli uliokataa mpira huo. Hofu ya kawaida ya kushuka tena iliwatawala, huku wakining’inia kulinda walichokuwa nacho, kitu walichokuwa wamekipoteza mara nyingi hapo awali.
Mashabiki walikuwa wakipuliza filimbi wakisubiri mateso hayo yaishe. Hatimaye, usiku wa Jumatano mwezi Mei, walijikuta wameachiwa mzigo mzito walioubeba kwa muda mrefu. Ramon Terrats, aliyekulia Espanyol, alipiga kichwa kuwapa bao. Kike Garcia, mshambuliaji mwenye umri wa miaka 36 anayejulikana kama “fundi wa mabao” ambaye alikuwa ameingia dakika sita tu kabla, alikimbilia mpira huo na kuupiga kwa utulivu ukampita kipa Unai Simon na kuwa bao. Saa ilisimama dakika 91:06 na ubao wa matokeo ukaonyesha 2-0. Na msimamo ukaonyesha Espanyol wako nafasi ya 14 wakiwa na pointi 42 na ushindi mara 11.
Mashabiki karibu 30,000 waliokuwa uwanjani walilipuka kwa furaha, huku kocha Gonzalez mwenyewe akishindwa kujizuia na kuangua kilio.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza tangu walipocheza na Athletic Club miezi mitano iliyopita. Tangu hapo, walikuwa wameingia kwenye kipindi kigumu wakicheza mechi 18 mwaka huu bila ushindi hata mmoja.
Wakati mmoja walikuwa wa nne mwezi Oktoba, wa tano mwanzoni mwa mwaka, na bado wa sita mwishoni mwa Februari. Lakini ndoto ya kucheza Ulaya iligeuka jinamizi la kushuka daraja. Walipata pointi sita kati ya 54, hali iliyowafanya wafike hatua ya kuamini hawawezi kushinda tena. Pere Milla, winga wa Espanyol alikiri kuwa, “ilifika wakati unaanza kuamini hutashinda tena. Hata mtoto wangu akija kucheza dhidi yetu tungepoteza.” Hata hivyo, kocha Gonzalez anasema: “Hatukustahili mateso yote haya, ila tulistahili ushindi huu.”
Hata hivyo, bado hakuna kilichokwisha katika msimu ambao umekuwa na vita kali zaidi ya kushuka daraja kuwahi kushuhudiwa La Liga. Pointi tatu tu zinatenganisha nafasi ya 12 hadi 19.
Kocha wa Athletic Club, Ernesto Valverde, anakiri kuwa bado ana hofu timu yake inaweza kushuka daraja licha ya kuwa nafasi ya tisa na Milla aliyefunga bao la kwanza kwa shuti kali kabla García hajamaliza kazi, alisema: “Tumepata ahueni kushinda, lakini bado hatujafanya chochote.”
Kwa kocha Gonzalez kipindi hiki kimekuwa kigumu kuliko hata maisha ya kawaida akisema: “Baada ya kifo cha mjomba wangu, hiki ndicho kipindi kigumu zaidi maishani mwangu.”
Kocha huyo mwenye hisia kali tangu utotoni ambaye aliwahi kuitwa Stoichkov (staa wa zamani Bulgaria – Hristo Stoichkov) kutokana na hasira na si kipaji, alikulia katika mazingira ya kawaida. Kabla hajawa kocha wa Espanyol, Garcia alikuwa akiendesha basi kutoka Badalona kwenda Barcelona kazi aliyofanya hadi 2018.
Alipopandishwa kutoka timu B kuwa kocha wa Espanyol 2024, jukumu hilo lilikuwa kama suala la maisha au kifo. Kama wasingepanda daraja, klabu ingeangamia. Kama wasingesalia La Liga, hali ingekuwa hiyo hiyo. Na msimu huu ulitakiwa uwe tofauti, lakini mateso yakarudi tena. Hakuna aliyeweza kuelewa jinsi timu hiyo ilivyoweza kucheza mechi 18 bila ushindi na kocha wa Athletic Club, Valverde, anasema: “Hili haliingii akilini.” Chuo Kikuu cha Vic cha Catalonia hata kilifanya utafiti kuhusu tatizo la kisaikolojia lililokuwa likiikumba Espanyol, wakichunguza namna walivyokuwa wakikosa kuhimili presha. Lakini, Espanyol hawakuwa peke yao kwenye mateso hayo.
Vita vya kushuka daraja La Liga vimekuwa vya kutisha kiasi kwamba timu 13 bado zinaweza kushuka huku mechi mbili zikiwa zimebaki. Pointi tano tu zinatenganisha nafasi za kucheza Ulaya na kushuka daraja. Levante walitoka kwenye eneo la kushuka daraja wiki hii baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidiya Celta Vigo ugenini, lakini wakajikuta wamerudi tena kwenye hatari juzi baada ya Sevilla kuishinda Villarreal 3-2 ikitoka nyuma kwa mabao mawili.
Nao Alaves waliigomea Barcelona wasiwafunge kwa mara ya kwanza katika mechi 54, huku Espanyol wakimaliza ukame uliowatesa kwa miezi mingi. Kwa sasa, Girona wako nafasi ya 19, Levante 18, Mallorca 17, Elche 16 na wote wakiwa na pointi 39. Alaves wana pointi 40, huku Espanyol, Valencia na Osasuna wakiwa nazo 42.
Kocha wa Sevilla, Luis García, anaiita hali hiyo ya kukosa mafanikio na kuumana katika msimamo kuwa ni “mashambulizi ya moyo kila mechi.”
Lakini kwa Gonzalez, angalau amepita katika wakati flani wa kupumua, akisema: “Imekuwa kama safari ya kuzimu. Ni vigumu kueleza. Tumekuwa tukicheza na maisha au kifo kila wiki. Familia yangu imeumia pamoja nami. Tumepunguza mzigo mkubwa mabegani mwetu. Labda nitapata usingizi mzuri kama Mungu alivyopanga.”