Habari za michezo
NANI NA NANI MCHUANO WA MCHEZAJI BORA EPL
Vardo
May 16, 2026
10:20 am
LONDON, ENGLAND: MASTAA walioteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora msimu wa Ligi Kuu England 2025-26 tayari imetolewa na wiki ijayo, Mei 23, mshindi anapatikana wakati michuano hiyo ikiwa katika hatua za mwisho na haya ndiyo majina wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo ya EA SPORTS Premier League Player of the Season 2025-26.
Washindi watano wanaowania tuzo hiyo walikuwa wanachezea timu zilizotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England huko nyuma. Mohamed Salah ndiye aliyeshinda tuzo ya mwisho ya POTS baada ya kuisaidia Liverpool kutwaa ubingwa wa 2024-25.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Misri hayupo katika orodha ya wachezaji wanane walioteuliwa safari hii. Erling Haaland ndiye mshindi wa zamani pekee aliyepo kwenye orodha ya walioteuliwa 2025-26.Je, mshambuliaji huyo wa Manchester City ataweza kuwa mchezaji wa sita kushinda tuzo hiyo mara mbili, au mmoja wa wengine saba ataibuka mshindi? Hapa chini tunachambua takwimu za kila mchezaji na sababu zinazowafanya kustahili kuwania tuzo EPL 2025-26.
BRUNO FERNANDEZ
Bruno Fernandes ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanane wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2020-21, baada ya kuwa na msimu bora akiwa Manchester United.
Fernandes anatarajiwa kumaliza msimu akiwa mchezaji mwenye pasi nyingi za mabao (asisti) kuliko wote kwenye ligi akiwa nazo 19 katika Ligi Kuu England 2025-26, akibakiza moja kufikia rekodi ya 20 iliyowekwa na Thierry Henry 2002-03 na Kevin De Bruyne 2019-20.
Asusti 10 kati ya 11 alizotoa zinatokana na mipira ya adhabu na kona, akiwa amebakiza moja kufikia rekodi ya Steven Gerrard 2013-14.
Kwa upande wa kutengeneza nafasi za mabao, Fernandes amekuwa juu kuliko mchezaji yeyote mwingine Ligi Kuu England, kwani tayari ametengeneza 124 za kufunga, kiwango chake bora tangu ajiunge na United, na kiwango bora zaidi kwenye ligi tangu Kevin De Bruyne alipotengeneza nafasi 136 msimu wa 2019-20.
Hakuna mchezaji wa Manchester United aliyewahi kushinda tuzo hiyo tangu Nemanja Vidic 2010-11, lakini United ndiyo klabu yenye washindi wengi zaidi wa tuzo hiyo katika misimu tofauti.
MORGAN GIBBS-WHITE
Morgan Gibbs-White amekuwa na msimu bora zaidi wa kufunga mabao katika Ligi Kuu England akifunga mabao 13 katika mechi 35 za Nottingham Forest.
Kwa ujumla, ni wachezaji watano pekee waliohusika katika mabao mengi zaidi ya yasiyo ya penalti kuliko yeye msimu huu. Pia ni mmoja wa wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi zaidi za wazi.
Kiungo huyo mshambuliaji pia aliisaidia Nottingham Forest kufika nusu fainali ya Europa League kabla ya kutolewa na Aston Villa.
Gibbs-White ni mmoja wa wachezaji wawili walioteuliwa mwaka huu ambao pia walikuwapo kwenye orodha ya mwisho msimu uliopita pamoja na Declan Rice.
Iwapo atashinda tuzo anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo akiwa kwenye timu iliyomaliza nusu ya chini ya msimamo tangu Juninho 1996-97 alipokuwa Middlesbrough.
ERLING HAALAND
Erling Haaland amewekwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo hiyo kwa mara ya tatu ndani ya misimu minne tangu ajiunge na Manchester City 2022.
Anaonekana kuwa karibu kushinda kiatu cha dhahabu kwa mara ya tatu akiwa tayari amefunga mabao 26 msimu huu – manne zaidi ya mpinzani wake wa karibu Igor Thiago.
Ni wachezaji wachache waliowahi kushinda kiatu cha dhahabu mara tatu au zaidi, akiwemo Thierry Henry, Mohamed Salah, Alan Shearer na Harry Kane.
Haaland ameendelea kuwa hatari mbele ya lango, huku pia akitoa asisti nane sawa na kiwango chake bora katika Ligi Kuu England. Anatafuta kushinda tuzo hiyo a mara ya pili baada ya 2022-23.
GABRIEL MAHALHAES
Gabriel Magalhães amekuwa mashine katika safu imara ya ulinzi ya Arsenal. Arsenal wamefungwa mabao 26 katika mechi 36 za msimu huu, na 19 tu kati ya hayo yalifungwa wakati Gabriel akiwa uwanjani.
Beki huyo huyo ni mmoja wa mabeki bora zaidi kwenye ligi akiwa na kiwango kizuri cha kushinda mipambano dhidi ya wapinzani. Nyota huyo anataka kuwa Mbrazili wa pili kushinda tangu Juninho 1996-97, na pia kuwa mmoja wa mabeki wachache waliowahi kushinda tuzo hiyo.
DAVID RAYA
David Raya tayari ameshinda tuzo ya Golden Glove ya Ligi Kuu England kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kutunza clean sheet 18 huku mechi mbili zikiwa zimebaki.
Kipa huyo wa Arsenal ndiye mchezaji pekee aliyeanza kila mechi ya ligi kwa kikosi cha Mikel Arteta msimu huu, bila kukosa hata dakika moja.
Iwapo atatunza clean sheet katika mechi mbili zilizobaki dhidi ya Burnley na Crystal Palace, atakuwa kipa wa kwanza tangu Alisson na Ederson 2021-22 kufikisha clean sheet 20 ndani ya msimu mmoja.
Raya anataka kuwa kipa wa pili kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England baada ya Peter Schmeichel 1995-96.
DECLAN RICE
Declan Rice yupo kwenye msimu wake wa tatu akiwa Arsenal, na ameingia kwenye orodha ya wanaowania tuzo hiyo katika misimu yote mitatu.
Hakuna mchezaji wa Arsenal wa nafasi ya nje aliyocheza dakika nyingi zaidi ya Rice msimu huu, akiwa amekosa mechi moja tu kati ya 36 za ligi.
Rice ndiye mchezaji aliyetengeneza nafasi nyingi zaidi Arsenal msimu huu, huku pia akiwa muhimu katika kuzuia mashambulizi na kurejesha umiliki wa mpira. Mchezaji wa mwisho wa Arsenal kushinda tuzo hiyo alikuwa Thierry Henry 2005-06.
ANTOINE SEMENYO
Antoine Semenyo alianza msimu akiwa Bournemouth, ambapo alihusika katika mabao 13 ndani ya mechi 20 kabla ya kuhamia Manchester City mwezi Januari.
Aliianza vyema maisha Man City akifunga katika mechi tano kati ya nane za kwanza Ligi kuu England. Kwa ujumla amefunga mabao 16 msimu huu na kutoa asisti nne. Nguvu kubwa ya Semenyo ni uwezo wa kukimbia na mpira kwa kasi.
Hakuna mchezaji aliyehusika katika mabao mengi zaidi yaliyotokana na kukokota mpira kuliko yeye msimu huu.
IGOR THIAGO
Baada ya msimu wa kwanza uliokuwa na majeraha mengi, Igor Thiago amekuwa mmoja wa mastaa wakubwa msimu huu akiwa Brentford.
Akiwa na mabao 22, tayari ameweka rekodi ya kuwa Mbrazili aliyefunga mabao mengi zaidi kwa Brentford katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England.
Mafanikio hayo yalisaidia kupata mwito wa kwanza kwenye timu ya taifa ya Brazil mwezi Machi. Thiago amefunga asilimia kubwa ya mabao ya Brentford msimu huu, huku pia akiwa mmoja wa washambuliaji wanaofanya kazi kubwa ya presha kwa wapinzani.
Pia ndiye mchezaji pekee aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu England zaidi ya mara moja msimu huu.