Habari za michezo
KOMBE LA DUNIA 2026 HALINOGI BILA SHAKIRA
Vardo
May 16, 2026
10:27 am
NI wanamuziki wengi wamepata nafasi ya kutumbuiza katika michuano ya Kombe la Dunia la FIFA lakini linapokuja suala la Shakira, 49, hii ni simulizi nzuri na refu inayohitaji muda wake wa kipekee ili kuisimulia vizuri.
Shakira, mzaliwa wa Colombia, tayari nimemshuhudia akitoa burudani katika fainali tatu za Kombe la Dunia, na ya nne tayari ipo mikono mwake, huku akiwa ameachia nyimbo tatu maalum za michuano hiyo ya kusisimua.
Katika Kombe la Dunia 2026 ambalo litaanza hivi karibuni katika nchi za Marekani, Canada na Mexico, tayari Shakira ameshatoa wimbo wake ‘Dai Dai’ akishirikiana na mshindi wa Grammy kutokea Nigeria, Burna Boy. Kutokana na ukubwa wa michuano hiyo na nguvu ya ushawishi aliyojenga Shakira juu yake, tunaenda kuangazia alichokifanya Kombe la Dunia katika msimu yote aliyopewa nafasi ya kushiriki kama mburudishaji.
1. Hips Don’t Lie – Ujerumani 2006
Katika fainali ya Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani ambayo iliwakutanisha Italia na Ufaransa katika uwanja wa Olympic jijini Berlin, Shakira alipata nafasi ya kutumbuiza kabla ya mechi hiyo. Mwimbaji huyo alitumbuiza kwa kushirikiana na Wyclef Jean, ambapo wawili hao waliimba pamoja wimbo wao, Hips Don’t Lie (2006) kutoka katika albamu ya saba yake Shakira, Oral Fixation, Vol. 2.
Hips Don’t Lie ni wimbo uliopata mafanikio makubwa duniani kote ukishika nafasi ya kwanza katika nchi 18, ikiwemo kwenye chati ya Billboard Hot 100 nchini Marekani, ukiwa ni wimbo wa kwanza wa Shakira kufanya hivyo.
Sasa Shakira na Wyclef Jean waliimba live wimbo huo katika sherehe ya kufunga mashindano hayo 2006, tukio ambalo watazamaji zaidi ya milioni 700 duniani kote walikuwa wakilifuatilia kupitia televisheni huku Italia ikitwaa Ubingwa.
2. Waka Waka – Afrika Kusini 2010
Katika ufunguzi wa Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini kwenye uwanja wa Orlando jijini Johannesburg, Shakira alitumbuiza wimbo wake maalumu kwa michuano hiyo, Waka Waka (This Time for Africa) (2010) ambao aliishirikisha bendi ya Freshlyground ya nchini humo.
Show hiyo ambayo ilipambwa pia na wasanii wengine kama Pitbull, Jennifer Lopez (J.Lo) na Claudia Leitte, kabla ya Shakira kuimba wimbo huo (Waka Waka), aliimba nyimbo zake maarufu kama Hips Don’t Lie (2006) na She Wolf (2009).
Haikuishia hapo, Shakira na Freshlyground Band walitumbuiza tena wimbo huo katika sherehe za kufunga mashindano hayo katika uwanja wa Soccer City, ambapo ilichezwa fainali kati ya Uholanzi na Hispania walioibuka mabingwa.
Waka Waka (This Time for Africa) (2010), ndio wimbo wa Shakira wenye mafanikio makubwa zaidi katika Kombe la Dunia, mathalani video yake imetazamwa (views) zaidi ya mara bilioni 4.5 YouTube ikiwa ni kazi yake ya kwanza kufikia namba hizo.
3. La La La – Brazil 2014
Hii ilikuwa mara ya pili kwa Shakira kuimba wimbo rasmi wa Kombe la Dunia, awamu hii akija na kibao chake, La La La (2014) ambacho alimshirikisha mwanamuziki maarufu kutokea Brazil, Carlinhos Brown. Alitumbuiza wimbo huo mbele ya mashabiki 74,738 wliojitokeza katika Uwanja wa Maracana, Rio de Janeiro, Brazil, kushuhudia fainali kati ya Argentina na Ujerumani walioibuka mabingwa kwa ushindi wa bao 1-0.
Video ya wimbo huo ambayo imeshatazamwa YouTube mara bilioni 1.3, imewaonyesha wachezaji mbalimbali kama Lionel Messi, Neymar, Cesc Fabregas, Sergio Aguero, Radamel Falcao, James Rodriguez, Eric Abidal, na aliyekuwa mpenzi wa Shakira wakati huo, Gerard Pique.
Mbali na Kombe la Dunia, video hiyo ilitengenezwa kwa ushirikiano na Activia kwa ajili ya kuunga mkono mpango wa kutoa chakula mashuleni wa World Food Programme, ambapo Shakira na Activia walitoa fedha kusaidia mpango huo.
4. Dai Dai – Marekani, Canada & Mexico 2026
Tayari imethitishwa kuwa Shakira atakuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2026 unaotarajiwa kupigwa katika uwanja wa MetLife huko New Jersey, Marekani hapo Julai 19. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Shakira, Madonna kutoka Marekani na kundi la BTS la Korea Kusini watafanya halftime show (burudani maalumu wakati wa mapumziko) ya kwanza kabisa katika historia ya fainali hizo.
“Halftime show ya fainali ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 itakuwa tukio maalumu sana litakalounganisha muziki, soka na dhamira ya pamoja ya kuboresha maisha ya watoto duniani kote,” anasema rais wa Fifa, Gianni Infantino kupitia mitandao ya kijamii.
Tayari Shakira na Burna Boy wametambulisha wimbo maalumu, Dai Dai (2026) ukiunga mkono Fifa Global Citizen Education Fund, mpango unalenga kukusanya Dola100 milioni (takriban Sh250 bilioni) hadi kufikia mwisho wa mashindano hayo ili kuwapatia watoto elimu bora na fursa za soka.