Habari za michezo

MAABAD AMVAA FEI TOTO

Vardo May 16, 2026 9:38 am

WAKATI Kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akifikisha mabao 11 na kuendelea kuongoza katika orodha ya wafungaji bora katika Ligi Kuu Bara, straika wa Coastal Union, Maabad Maulid amesema hata yeye anakiwinda kiatu cha ufungaji bora msimu huu.

Maabad aliyejiunga na Wagosi hao misimu miwili nyuma akitokea KVZ ya Zanzibar, anakumbukwa kwa rekodi aliyoacha katika Ligi Kuu Zanzibar alipoibuka mfungaji bora kwa mabao 19 na kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo msimu wa 2021-2022.

Kwa muda wote aliotumikia Coastal Union, ameendelea kuaminiwa kikosini licha ya ushindani wa namba uliopo huku akiwa na mwendelezo mzuri wa kuwa kinara wa mabao kikosini muda wote.

Akizungumza na Soka la Bongo, Maabad mwenye mabao matano katika Ligi Kuu Bara msimu huu, amekiri ugumu wa ligi hiyo akieleza kuwa matokeo waliyonayo hivi sasa haikuwa matarajio yao akitoa matumaini kuwa Coastal Union itabaki salama.

Amesema licha ya ushindani wa namba kikosini, lakini kuaminiwa na benchi la ufundi inampa nguvu na hamasa kubwa katika kuendelea kupigania ndoto yake ya kusaka kiatu cha mfungaji bora.

“Ligi Kuu Bara ni ngumu sana ukilinganisha na Zanzibar, lakini bado sijajikatia tamaa kwakuwa tunayo michezo saba imebaki na inaweza kuamua lolote katika safari yangu, kimsingi najipanga kutumia nafasi niwapo uwanjani,” amesema Maabad.

Nyota huyo ameongeza kuwa, bado hawaridhishwi na kasi ya ufungaji mabao kikosini akieleza kuwa malengo zaidi ni kuona timu hiyo inapata matokeo mazuri na kuwaomba wenzake kuendelea kupambana.

ERIC MWIJAGE KATIKA RADA ZA PAMBA JIJI BEIMBAYA APATA MATUMAINI MAPYA B19 FC