Habari za michezo
ERIC MWIJAGE KATIKA RADA ZA PAMBA JIJI
Vardo
May 16, 2026
9:32 am
MABOSI wa Pamba Jiji wameanza kuweka mikakati ya mapema ya kujiimarisha kwa msimu ujao wakimuweka kwenye rada winga wa KMC, Erick Mwijage huku wakisubiri hatma ya timu hiyo kwenye mbio za kubaki Ligi Kuu Bara.
Taarifa za ndani zilieleza kuwa, Pamba ipo tayari kufanya mazungumzo rasmi ya kumchukua Mwijage endapo KMC itashuka daraja mwishoni mwa msimu huu, wakiamini nyota huyo anaweza kuongeza ushindani mkubwa kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Mwijage amekuwa mmoja wa wachezaji wanaotazamwa zaidi ndani ya KMC kutokana na uwezo wake wa kucheza pembeni kwa kasi, kutengeneza nafasi na kusaidia mashambulizi ya kushtukiza jambo ambalo limevutia benchi la ufundi la Pamba.
Chanzo kutoka ndani ya Pamba kililiambia Soka la Bongo kuwa, viongozi wa timu hiyo wanaamini usajili wa Mwijage utawapa nguvu kubwa eneo la mawinga ambalo wanataka kuliboresha kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.
Taarifa hizo zilisema kuwa, mpango mkubwa wa Pamba ni kumtumia Mwijage sambamba na kiungo mshambuliaji John Nakibinge ili kuongeza ubunifu na kasi kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji wa timu hiyo.
“Mbali na uwezo wake wa kushambulia, Mwijage pia ameonekana kuwa na nidhamu nzuri ya uwanjani na uwezo wa kucheza mifumo tofauti jambo linalomfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaowindwa na Pamba kwa sasa,” kimesema chanzo.
Kwa upande wa KMC, bado haijaweka wazi hatma ya baadhi ya nyota wake huku vita ya kubaki ligi kuu ikiendelea kushika kasi, lakini inaelezwa kuwa baadhi ya timu tayari zimeanza kuwafuatilia wachezaji wao muhimu kabla ya dirisha kubwa la usajili kufunguliwa.
Pamba yenyewe imeonyesha dhamira ya kufanya vizuri zaidi msimu ujao baada ya maboresho mbalimbali yanayoendelea ndani ya kikosi hicho, huku viongozi wakiamini kuongeza wachezaji wenye uzoefu wa Ligi Kuu Bara kutawasaidia kufikia malengo yao mapya.
KMC inapumulia mashine ikiwa mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya alama tisa kwenye mechi 23 ilizocheza, zikibaki saba kujitetea isishuke.