Habari za michezo

CHAMA AUWASHA MOTO, SIMBA IKITINGA NUSU FAINALI CRDB FEDERATION CUP

Vardo May 17, 2026 10:49 pm

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama, ameendelea kuonyesha kiwango bora msimu huu baada ya kufunga katika mchezo wa tano mfululizo na kuisaidia timu hiyo kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Simba imepata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya TRA United katika mchezo uliochezwa leo Jumapili Mei 17, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Chama alianza kuonyesha ubora wake mapema baada ya kuifungia Simba bao dakika ya sita, kufuatia mashambulizi ya kasi yaliyowapa wakati mgumu wapinzani wao.

Bao hilo limeendelea kuthibitisha kiwango kikubwa cha kiungo huyo ambaye katika michezo minne iliyopita ya Ligi Kuu Bara amefunga matano na kutoa asisti mbili.

Simba ilionekana kutawala mchezo tangu mwanzo huku safu ya ushambuliaji ikiwabana TRA United kwa kutengeneza presha wakati wakiwa hawana mpira jambo lililowafanya kushindwa kucheza kwa utulivu.

Baada ya kuruhusu bao la mapema, TRA United ilijaribu kujibu mashambulizi kwa kutumia zaidi maeneo ya pembeni, hasa upande wa kulia aliokuwa akicheza Ramadhan Salum ‘Chombwedo’.

Hata hivyo, juhudi hizo hazikuzaa matunda kwani safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa imara na kuwazuia wapinzani wao kutengeneza nafasi za hatari.

Wakati TRA ikisaka bao la kusawazisha, Simba iliongeza la pili dakika ya 26 kupitia kwa Anicent Oura.

Bao hilo liliwapa Simba utulivu mkubwa ndani ya mchezo huku TRA United ikionekana kupoteza mwelekeo kutokana na presha ya mabao mawili ya kipindi cha kwanza. Mpaka mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa TRA United kuonyesha nidhamu kubwa zaidi ya ulinzi katika dakika 15 za kwanza tofauti na ilivyokuwa kipindi cha kwanza ambapo ilionekana kuruhusu nafasi nyingi.

Mabadiliko hayo yaliifanya Simba kupata ugumu wa kupenya kirahisi kwenye eneo la hatari kutokana na wapinzani wao kujaza wachezaji wengi nyuma.

Licha ya ugumu huo, Simba iliendelea kutawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga kupitia viungo na washambuliaji waliokuwa wakibadilishana nafasi.

Bao la tatu la Simba lilifungwa na Seleman Mwalimu aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Oura huku Bashiri Kibaila ambaye naye aliingia kuchukua nafasi Libasse Guaye akifunga la nne lililohitimisha matumaini ya TRA United kurejea mchezoni.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefuzu hatua ya nusu fainali ambapo itakutana na Coastal Union ya Tanga iliyowatoa Singida Black Stars kwa penalti 4-2 baada ya sare ya bila mabao.

Kabla ya mchezo huo wa nusu fainali, Simba itakuwa na kibarua kingine dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Mei 21 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Nusu fainali itakuwa kati ya Juni 20 na 21 mwaka huu.

BRUNO ABAKISHA DAKIKA 90 KUWEKA REKODI MPYA EPL MAMELODI YAANZA VIZURU HESABU ZA UBINGWA CAF