Habari za michezo
BRUNO ABAKISHA DAKIKA 90 KUWEKA REKODI MPYA EPL
Vardo
May 17, 2026
10:43 pm
MANCHESTER, ENGLAND: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes ameifikia rekodi ya pasi nyingi za mabao katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England baada ya kikosi hicho kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Nottingham Forest, ukiwa ni mchezo uliokuwa wa kusisimua uliozaa mabao matano. Wafungaji wa Man United ni Luke Shaw (dk 5), Matheus Cunha (dk 55) na Bryan Mbeumo (dk 76). Yale ya Nottingham Forest yalifungwa na Morato (dk 53) na Morgan Gibbs-White (dk 78).
Fernandes amefikisha pasi 20 za mabao msimu huu baada ya krosi yake kutoka upande wa kulia kumkuta Bryan Mbeumo aliyefunga bao la tatu la United, hivyo kumfanya nahodha huyo kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Thierry Henry (2002–03) na Kevin De Bruyne (2019–20). Akiwa na mchezo mmoja pekee uliobaki msimu huu sawa na dakika tisini, Fernandes bado ana nafasi ya kuweka rekodi mpya.
Katika siku ambayo Casemiro alipigiwa makofi ya heshima na mashabiki wa Old Trafford wakati wa kuaga dakika tisa kabla ya mchezo kumalizika, Manchester United ilipata matokeo muhimu yaliyowahakikishia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi chini ya kocha Michael Carrick.
Mafanikio ya Fernandes yalisaidia kupunguza mjadala mkubwa uliotokana na tukio lingine tata la VAR.
Nottingham Forest walikuwa wametoka kusawazisha bao la mapema la Luke Shaw la dakika ya tano kupitia kichwa cha Morato, ndipo Diogo Dalot alipotoa krosi iliyomfikia Mbeumo.
Mshambuliaji huyo wa Cameroon alionekana kuudhibiti mpira kwa sehemu ya mkono wa juu kabla ya shuti lake kuzuia na mpira kuelekea kwa Matheus Cunha aliyemalizia kwa shuti lililojaa wavuni.
Mwamuzi Michael Salisbury alikubali bao hilo tangu mwanzo, lakini baada ya kuitwa na mwamuzi wa VAR, Matthew Donohue kwenda kuangalia tukio hilo kwenye skrini, wengi walitarajia lingefutwa.
Hata hivyo, baada ya ukaguzi wa muda mrefu uliosababisha mashabiki wa pande zote mbili kupiga kelele za kutoridhishwa kutokana na kuchelewa kwa uamuzi, Salisbury alithibitisha bao hilo, akieleza kuwa mpira ulikuwa umegonga nyonga ya Mbeumo badala ya mkono.
Dakika 12 kabla ya mchezo kumalizika, Morgan Gibbs-White aliifungia Forest bao la pili, lakini wageni hao walishindwa kupata bao la kusawazisha.
Katika mechi hiyo ya mwisho msimu huu kuchezwa Old Trafford, kulikuwa na matukio mengine ya kukumbukwa.
Luke Shaw alionekana kushangazwa hata yeye mwenyewe baada ya kufunga bao lake la mapema. Haikuwa jambo la kushangaza, kwani bao lake la mwisho la Ligi Kuu England lilikuwa dhidi ya Bournemouth Januari 2023, na hilo likiwa bao lake la tano pekee katika mashindano yote akiwa na Manchester United.
Fernandes tayari alikuwa ameshindwa kufikisha pasi yake ya 20 katika michezo miwili iliyopita. Wakati Mbeumo alipokosa nafasi nzuri aliyotengenezewa na kiungo huyo wa Ureno, Fernandes alionekana kujitupa chini kwa huzuni, kana kwamba alihofia rekodi hiyo isingefikiwa.
Hatimaye, baada ya Mbeumo kukosa nafasi nyingine kwa kupiga mpira uliogonga mwamba wa lango katika kipindi cha kwanza, huku akiendelea kusota bila bao tangu Februari 7 mwaka huu, pasi ya Fernandes ilimfikia na kufunga, hali iliyosababisha wachezaji wa United kusherehekea kwa furaha kubwa huku wengi wakimkimbilia nahodha wao kabla hata ya kumpongeza mfungaji.
Fernandes angeweza kuandika rekodi ya pasi za mabao katika mechi hiyo, lakini Diogo Dalot alipiga shuti lililogonga mwamba katika dakika za nyongeza na kushindwa kufunga.
Hata hivyo, tukio lililowavuta zaidi mashabiki lilikuwa la Casemiro.
Kiungo huyo wa Brazil alionekana kuguswa sana alipokuwa akitoka uwanjani polepole baada ya nafasi yake kuchukuliwa na Mason Mount dakika tisa kabla ya mechi kumalizika, huku akipeana mikono na wachezaji wenzake akienda benchi.
Joshua Zirkzee naye alikaribia kuongeza bao mwishoni mwa mchezo, lakini kipa wa Forest, Matz Sels, alikaa imara kuzuia shambulizi hilo.
Fernandes anaweza kuandika rekodi mpya ya pasi nyingi za mabao katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England kwenye mechi ya mwisho ambayo United itakuwa ugenini kucheza Brighton, Mei 24 mwaka huu.