Habari za michezo

KABLA YA KUWAVAA TRA UNITED, MO DEWJI AIBADILISHA KAMBI YA SIMBA SC

Vardo May 17, 2026 10:20 pm

KUELEKEA robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kati ya Simba SC na TRA United, klabu ya Simba imepata chachu mpya ya morali baada ya Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (Mo Dewji), kufika kambini kuzungumza na kikosi hicho.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa itapigwa leo katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo Simba wanashuka dimbani wakiwa na lengo moja kuu ni kufuzu hatua ya nusu fainali na kuendelea kusaka ubingwa wa mashindano hayo.

Mo Dewji aliwasili kambini katika wakati muhimu kabisa kwa timu hiyo, ambapo alikutana moja kwa moja na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

Lengo lake lilikuwa kuwapa hamasa na kuwakumbusha uzito wa mchezo huo, ambao unaweza kuamua hatma ya safari yao katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Mazungumzo hayo yameelezwa kufanyika katika mazingira ya kuhamasisha zaidi kuliko maonyo, ambapo viongozi na wachezaji walipata nafasi ya kujiandaa kisaikolojia kabla ya pambano hilo muhimu. Simba wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kila mchezo, huku wakijua hakuna nafasi ya makosa katika hatua za mtoano

Akizungumza kupitia Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema ujio wa Mo Dewji umeongeza nguvu mpya na ari kubwa ndani ya kikosi hicho kuelekea mchezo dhidi ya TRA United.

“Bhaaaaaassssssiii wamekwisha, leo Rais wa heshima amekutana na wachezaji na benchi la ufundi kuzungumza nao kabla ya mchezo wetu dhidi ya TRA,” alinukuliwa Ahmed Ally, akisisitiza namna morali ilivyopanda kambini baada ya mkutano huo.

Simba sasa wanaingia uwanjani wakiwa na nguvu mpya na motisha ya ziada kutoka kwa uongozi, huku mashabiki wakisubiri kuona kama hamasa hiyo itatafsiriwa kuwa matokeo chanya dhidi ya TRA United katika pambano hilo la robo fainali.

MAEMA NA MUSTAKABALI WAKE SIMBA, VITA YA SAINI YAZIDI KUPAMBA MOTO BRUNO ABAKISHA DAKIKA 90 KUWEKA REKODI MPYA EPL