Habari za michezo

MAEMA NA MUSTAKABALI WAKE SIMBA, VITA YA SAINI YAZIDI KUPAMBA MOTO

Vardo May 17, 2026 3:10 pm

KIUNGO mshambuliaji raia wa Afrika Kusini, Neo Maema, amejikuta akiwa kwenye ukurasa mpya wa mustakabali wake baada ya muda wake wa mkopo ndani ya Simba SC kukaribia kufikia tamati, hali inayozidi kuibua mjadala mkali kuhusu hatma yake Msimbazi.

Maema, alijiunga na Simba SC kwa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns, na tangu kuwasili kwake amekuwa miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika kuongeza ubunifu na kasi kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Akiwa uwanjani, Maema ameonekana kuwa kiungo mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi na kuunganisha safu ya kati na washambuliaji, jambo lililomfanya kuwa chaguo muhimu katika mipango ya benchi la ufundi la Simba.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu, mkataba wa mkopo wa nyota huyo unatarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu huu, hivyo Simba italazimika kuingia mezani na mazungumzo mapya iwapo inataka kumbakiza Msimbazi.

Hata hivyo, changamoto kubwa ni kwamba Maema bado ana mkataba wa muda mrefu na Mamelodi Sundowns unaoendelea hadi Juni 30, 2026, hali inayowapa Waafrika Kusini nguvu kubwa katika maamuzi ya hatma yake.

Hali hiyo imeifanya safari ya kumbakiza kiungo huyo kuwa ngumu zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa sio Simba pekee inayomuwania, bali pia kuna klabu nyingine kutoka Afrika Kusini zinazomwona kama chaguo muhimu kwa msimu ujao.

Uongozi wa Simba umeelezwa kuwa na nia ya dhati ya kumbakiza Maema kutokana na kiwango chake na mchango wake uwanjani, lakini sasa unakabiliwa na ushindani mkali wa soko la usajili ambalo linazidi kuwa na mvuto kwa nyota huyo.

Hatma ya Maema inatarajiwa kujulikana baada ya mazungumzo rasmi kati ya pande husika, huku mashabiki wa Simba wakisubiri kwa hamu kuona kama ataendelea kung’ara Msimbazi au atarejea Afrika Kusini kuanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka.

MUDATHIR AWASHTUKIA MASHABIKI KISA MWAMNYETO