SAN ANTONIO, TEXAS: TIMU ya San Antonio Spurs imeanza safari ya kujenga uwanja mpya wa kisasa wenye thamani ya Dola 1.3 bilioni (zaidi ya Sh.3.39 trilioni), mradi unaoonekana kuendana na zama mpya za nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Victor Wembanyama katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA).
Kupitia kampuni mama ya Spurs Sports & Entertainment (SS&E), uongozi wa klabu hiyo umetangaza kundi la wataalamu na kampuni tisa zitakazosimamia mradi huo mkubwa unaotarajiwa kukamilika ifikapo 2032 katikati ya Jiji la San Antonio.
Mradi huo sio kwa ajili ya kujenga uwanja pekee, bali pia unahusisha maendeleo ya eneo kubwa la biashara, burudani na huduma za kijamii. Hii ni sehemu ya mpango mpana wa kuifanya San Antonio kuwa moja ya vituo vikubwa vya michezo na biashara nchini Marekani.
Uamuzi huo umefanywa katika kipindi ambacho umaarufu wa Wembanyama umeendelea kukua kwa kasi duniani.
Nyota huyo mwenye urefu wa futi 7 na inchi 4 (takribani mita 2.24) ameigeuza San Antonio Spurs kuwa moja ya timu zinazofuatiliwa zaidi NBA huku kiwango chake kikitajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za kufanya kuwepo kwa mradi huo mkubwa wa kifedha.
Katika msimu wa NBA wa 2025/26, Wembanyama ameendelea kuthibitisha kuwa sura mpya ya ligi hiyo baada ya kuongoza tena kwa kupiga ‘blocks’ yani kuzuia mara nyingi kwa msimu wa tatu mfululizo sambamba na wastani wa zaidi ya pointi 25 kwa kila mchezo.
Kutokana na ushawishi wake mkubwa kibiashara na kimichezo, Spurs wanaonekana kujenga mazingira yatakayoendana na hadhi ya mchezaji huyo ambaye tayari wengi wanamuona kuwa mrithi wa mastaa waliowahi kutawala NBA akiwemo LeBron James na Michael Jordan.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa SS&E, RC Buford alisema wamechagua washirika wenye uwezo mkubwa kimataifa lakini pia wanaoifahamu vizuri San Antonio ili kuhakikisha mradi huo unaleta faida kwa jamii pamoja na kuiwakilisha vizuri historia ya mji huo.
Miongoni mwa kampuni zilizochaguliwa ni CAA Icon ambao wamewahi kusimamia ujenzi wa viwanja maarufu vya michezo Marekani huku kampuni ya Overland International ikipewa jukumu la kubuni mwonekano wa uwanja huo mpya.
Pia kampuni ya Sasaki itasimamia upangaji wa eneo lote la ekari 25 ambapo utajengwa uwanja huo, eneo ambalo linatarajiwa kuwa kitovu kipya cha burudani, biashara na utalii. Hata hivyo, pamoja na msisimko mkubwa wa mashabiki wa Spurs mradi huo umeanza kukumbana na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wadau wa jiji hilo.
Ripoti zinaonyesha kuwa karibu Dola 10 milioni (zaidi ya Sh25.8 bilioni) tayari zimetumika kwa gharama za ushauri na mipango kabla hata eneo rasmi la ujenzi kununuliwa, jambo lililoibua maswali kuhusu matumizi ya fedha za umma katika hatua za mwanzo za mradi huo.
Baraza la Jiji la San Antonio pia limekubali kutoa zaidi ya Dola 6 milioni (zaidi ya Sh15.69 bilioni) kwa huduma za ushauri kupitia mpango maalumu unaoitwa ‘Project Marvel’. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo, Spurs watachangia Dola 500 milioni ambazo ni zaidi ya Sh1.3 trilioni katika mradi huo huku wakibeba mzigo wa gharama zozote zitakazozidi bajeti iliyopangwa.
Pamoja na lawama hizo, wachambuzi wengi wa NBA wanaamini Spurs hawana chaguo zaidi ya kuwekeza kwa kiwango kikubwa kutokana na nafasi ya kipekee waliyonayo kupitia Wembanyama. Tayari nyota huyo ameifanya San Antonio kurejea kwenye ramani ya ushindani wa NBA, huku ikiwa katika vita vya hatua ya nusu fainali ya Kanda ya Magharibi dhidi ya Minnesota Timberwolves.
Mahitaji ya kuwa na uwanja wa kisasa yanaonekana kuongezeka kadri umaarufu wa Spurs unavyoongezeka duniani, hasa kupitia mauzo ya tiketi, jezi, matangazo na haki za biashara zinazohusiana na Wembanyama.