BONDIA chipukizi wa uzani wa kilo 60, Abubakar Mdose, ni miongoni mwa vijana wanaopambana kutimiza ndoto za kufika mbali katika mchezo wa ngumi nchini.
Mdose, anayefanya mazoezi katika gym ya National Punch Boxing Club iliyopo Mabibo, Dar es Salaam, chini ya makocha Hashim Polopela na Juma Shomvi, anasema safari yake ya ngumi imekuwa na changamoto, lakini moyo wa kupambana umeendelea kumfanya asonge mbele.
Soka la Bongo lilifanya mahojiano na bondia huyo kujua safari yake, kwanini ngumi na sio mchezo mwingine pamoja na malengo yake.
ALIANZAJE?
Mdose anasema alianza kujifunza ngumi tangu akiwa kijana mdogo, lakini rasmi kuingia ulingoni ilikuwa mwaka 2022, akivutiwa na mafanikio ya mabondia mbalimbali nchini na anaamini kupitia wao anaweza kufika mbali.
“Hapa nafanya mazoezi chini ya kocha Hashim Polopela na Juma Shomvi. Wamekuwa msaada mkubwa sana kwangu tangu nilipoanza safari yangu mwaka 2018,” anasema Mdose.
Anaeleza kuwa kutokana na kuupenda mchezo huo alifikia wakati hapumziki akitoka shule anaingia moja kwa moja mazoezini ili ndoto yake ya kupanda ulingoni itimie.
“Maisha yangu ya boxing yalikuwa magumu. Nilikuwa natoka shule Makongo Vocational Training Center na kwenda moja kwa moja mazoezini bila hata kurudi nyumbani kula. Ilikuwa ni hali ngumu, lakini nilijua nilichokuwa nakitafuta,” anasema
“Licha ya kupambania kipaji changu mama yangu na familia yangu wananisapoti sana ili nitimize ndoto zangu. Wanahakikisha ninapata kila mahitaji yaliyokuwa chini ya uwezo wao,” anasema
Bondia huyo alisema kuna wakati aliwahi kukata tamaa na kufikiria kuachana na mchezo huo, lakini alibadili uamuzi baada ya kupata ushauri kutoka kwa bondia mwenzake, Mohamed Rashid.
“Nilifika mahali nikawa na mawazo ya kuacha. Kilichonirudisha ni mawazo mazuri na ushauri bora kutoka kwa Mohamed Rashid maarufu kama Mudy Pesa alinieleza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu.”
Mbali na familia yake, Mdose alisema pia amekuwa akipata sapoti kubwa kutoka kwa watu wa mtaani kwao wanaomtia moyo kuendelea kupigania ndoto zake.
“Mitaa niliyotokea inanisaidia sana. Nilihimizwa niendelee kupeperusha bendera, na pia nilipata sapoti kubwa kutoka kwa Allen Yonaza, maarufu kama Mabonye, ambaye amenisaidia kufikia malengo yangu,” anasema.
CHANGAMOTO
Bondia huyo anasema moja ya changamoto kubwa kwenye mchezo wa ngumi ni malipo ya uhakika wanapopigana hususani mabondia chipukizi ambao wanajitafuta.
“Mabondia wengi tunacheza mapambano bila kupata malipo ya pambano. Hii ni changamoto kubwa kwa sababu maandalizi yanahitaji muda, nguvu na gharama,” anasema Mdose na kuongeza.
“Kuna mapromota anakwambia kuna pambano labda sehemu fulani unajiandaa vizuri, muda mwingine bondia anakopa hadi pesa kwa ajili ya maandalizi ukimaliza pambano humuoni na hujui unamtafutia wapi hii ni changamoto kubwa,”
Licha ya changamoto hizo, bondia huyo anasema bado ana ari kubwa ya kuendelea kupambana na kutengeneza rekodi nzuri itakayomfungulia fursa za mapambano makubwa zaidi.
REKODI ZAKE
Mdose anapigana katika uzani wa kilo 60 na tayari ameanza kujitengenezea jina katika medani ya ngumi za kulipwa nchini.
Kwa mujibu wa takwimu za Boxrec bondia huyo ameshacheza mapambano manne, akishinda matatu na kupoteza moja. Kwenye mapambano ya ushindi aliwafunga Selestine Martine wa Mbezi Beach, Nawaw Qudus wa Tandale Manyara na Hashim Shen wa Kigamboni Dege.
Pambano pekee alilopoteza ni dhidi ya Patrick Paul wa Chunya, mkoani Mbeya, pambano ambalo anasema limempa uzoefu mkubwa.
“Kila pambano lina fundisho. Kushindwa kwangu dhidi ya Patrick Paul kulinifanya nijue maeneo ya kuboresha na kunifanya nirudi gym kwa nguvu zaidi. Mapambano manne ni mwanzo. Ninaamini bado nina nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi na kufikia viwango vya juu,” anasema.
PAMBANO LA KWANZA
Mdose anasema pambano lake la kwanza kupanda ulingoni lilikuwa mwaka 2022 dhidi ya Abdallah Ponda. Alisema wakati huo hakuwa na uzoefu mkubwa wa mashindano, jambo lililomfanya kushindwa kuonyesha uwezo mzuri.
Anaeleza kuwa kipigo hicho kilimpa funzo kubwa kuhusu nidhamu, maandalizi na umuhimu wa kujiamini akiwa ulingoni.
Kwa mujibu wa Mdose, matokeo hayo hayakumvunja moyo, bali yalikuwa mwanzo wa safari ya kujifunza.
“Sikufanya vizuri kama nilivyotarajia na nikapoteza kwa pointi, lakini matokeo hayo hayakunivunja moyo. Badala yake, yalinipa somo kubwa na kunifanya nijitume zaidi mazoezini, jambo lililonisaidia kushinda mapambano matatu yaliyofuata.”
NDOTO ZAKE NA ANAOWATAZAMA
Bondia huyo anasema ndoto yake kubwa ni kuwa bingwa wa taifa na baadaye kushindania mikanda ya kimataifa.
“Nataka kuwa bingwa wa Tanzania, Afrika na hata dunia. Ndoto yangu ni kuona jina langu likitajwa katika mapambano makubwa na kuwakilisha nchi yangu,” anasema bondia huyo na kuongeza kwamba anawatazama mabondia watatu nchini na anatamani kufikia uwezo ambao ni Mohamed Mudy pesa, Ally Mwirange na Emmanuel Mwakyembe.
Anataja sababu kwanini amechagua mabondia hao kama kioo chake na si wengine kama Hassan Mwakinyo, Dullah Mbabe wanaofanya vizuri na kuwakilisha kimataifa.
“Kwanza hao ni washauri wangu wakubwa pia ni mabondia wazuri mfano Mwakyembe anapigana sana, ana punch nzuri, ana nguvu pia ana pumzi nzuri,” anasema.