Habari za michezo

PRESHA YAZIDI KWA MWAMNYETO, AOMBA KUPUMZISHWA

Vardo May 17, 2026 9:37 am

MSEMAJI wa klabu ya Young Africans SC, Ali Kamwe, amesema nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, amekosa mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania kutokana na kutokuwa sawa kisaikolojia baada ya kupokea jumbe nyingi zenye mashinikizo na matusi kupitia simu yake binafsi.

Kamwe amesema tangu baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC, Mwamnyeto alianza kupokea ujumbe mzito kutoka kwa baadhi ya mashabiki, hali iliyomwathiri kiakili na kumfanya ashindwe kuwa tayari kwa mchezo huo wa robo fainali.

Ameeleza kuwa beki huyo hana tatizo lolote la majeraha, bali mwenyewe aliwasiliana na benchi la ufundi na kuomba kupumzishwa ili kupata muda wa kurejea katika hali nzuri kiakili kabla ya kurejea tena uwanjani kuitumikia timu yake.

Kwa mujibu wa Kamwe, baadhi ya mashabiki walienda mbali zaidi kwa kuwatafuta hata ndugu wa Mwamnyeto na kuwatumia jumbe za matusi, jambo alilosema si la kibinadamu na linaweza kumuathiri mchezaji yeyote anayepitia presha kubwa ya mashindano.

“Tumemkosa si kwa sababu ya majeraha, bali hayupo sawa kichwani hivyo aliomba benchi la ufundi apumzike kwenye mchezo huu. Ni jukumu la kila Mwanayanga kusimama na wachezaji hata siku wanapokuwa hawajacheza vizuri,” amesema Kamwe.

Kamwe amewataka mashabiki kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wao katika nyakati zote, akisisitiza kuwa soka lina ushindi na changamoto zake, hivyo wachezaji wanahitaji faraja na sapoti kutoka kwa mashabiki badala ya kushambuliwa kwa maneno yanayoweza kuwaumiza kisaikolojia.

BLACK STARS YA KINA SEMENYO KUIFUTA REKODI YA ESSIEN MANGUNGU AWEKA WAZI SIRI YA MABADILIKO SIMBA