Habari za michezo
BLACK STARS YA KINA SEMENYO KUIFUTA REKODI YA ESSIEN
Vardo
May 17, 2026
9:32 am
ACCRA, GHANA: Tangu ilipofuzu kwa mara ya kwanza kwa Kombe la Dunia 2006, Ghana imeshindwa kufuzu kucheza fainali hizo mara moja tu 2018, lakini tatizo ni mwendo wa kusuasua kwa siku za karibuni pamoja na migogoro ya ndani ya soka lao jambo linalozua hofu juu ya hatma yao kwa fainali za mwaka huu ambazo zinaandaliwa na Marekani, Canada na Mexico.
Uamuzi wa kuachana na kocha wao Otto Addo siku 72, kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia umeibua hofu na shaka juu ya hatma yao. Shaka hiyo ipo kwa Black Stars kuelekea mchezo wake wa kwanza dhidi ya Panama, unaonekana kuwa ni mwepesi kwao kabla ya kuivaa timu zinazopewa nafasi kubwa katika fainali hizo England na Croatia.
Tumaini pekee la Ghana dhaifu linabebwa na nyota wake Antoine Semenyo, lakini mchezaji huyo wa Manchester City anahitaji kupata ushirikiano kutoka kwa wenzake ili kukwepa aibu katika fainali hizo.
Pamoja na kushindwa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika AFCON, hivi karibuni, lakini Ghana ilifanikiwa kufuzu Kombe la Dunia wakiwa vinara katika kundi lake wakishinda mechi nane kati ya kumi na kuwafanya kumaliza wakiwa vinara kwa tofauti ya pointi sita. Mshambuliaji wake mkongwe Jordan Ayew mwenye miaka 34, anayecheza timu ya daraja la pili ya Leicester City, katika mechi za kufuzu alifanikiwa kufunga mabao saba na kuipa Ghana tiketi ya kwenda kwenye fainali hizo.
Taifa hilo la Afrika Magharibi ni moja ya timu zilizobeba hadhi ya bara hili katika mashindano ya kimataifa kwa zaidi ya nusu karne. Kuanzia zama za kina Abedi Pele, Tony Yeboah, Asamoah Gyan, Jordan Ayew hadi kizazi cha Mohammed Kudus na Antoine Semenyo, Ghana imeendelea kuwa moja ya nchi zenye historia kubwa zaidi ya soka Afrika. Sasa macho yao yote yapo katika fainali za Kombe la Dunia 2026.
Baada ya miamba hiyo kukosa fainali zilizopita za AFCON 2025, wanakwenda Marekani wakiwa na kiu ya kurudisha heshima yao.
HISTORIA KUBWA YA GHANA
Ghana ni moja ya mataifa yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya soka la Afrika. Imeshinda mataji manne ya AFCON 1963, 1965, 1978 na 1982. Huku mafanikio yake makubwa zaidi katika Kombe la Dunia ni kucheza robo fainali mwaka 2010.
Katika miaka ya 1960, Ghana ilikuwa chini ya kocha nguli Charles Kumi Gyamfi ambaye aliiongoza timu hiyo kutawala soka la Afrika. Chini yake, Ghana ilicheza soka la kuvutia, lenye nidhamu na kasi, jambo lililoifanya kuwa miongoni mwa timu za kwanza kabisa za Afrika kuheshimiwa duniani. Lakini mafanikio hayo hayakuishia Afrika pekee. Ghana pia imekuwa taifa lenye historia kubwa katika mashindano ya vijana. Mwaka 2009 waliweka historia kwa kuwa taifa la kwanza Afrika kushinda Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 20 baada ya kuifunga Brazil katika fainali zilizofanyika nchini Misri. Kizazi hicho kilikuwa msingi wa mafanikio yao katika Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.
GHANA NA KOMBE LA DUNIA
Ghana ilifuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2006 nchini Ujerumani na kufanikiwa kufika hatua ya 16 bora alipotolewa na Brazil na kuandika rekodi ya kuwa timu pekee ya Afrika kuvuka hatua ya makundi katika mashindano hayo.
Walikuwa na kikosi chenye vijana wengi wakiongozwa na Asamoah Gyan, Stephen Appiah, Sulley Muntari na Michael Essien.
Lakini mafanikio makubwa zaidi yalikuja mwaka 2010 nchini Afrika Kusini. Ghana ilifika robo fainali na kuwa taifa la tatu Afrika kufanya hivyo baada ya Cameroon na Senegal. Mechi yao dhidi ya Uruguay imeendelea kukumbukwa milele katika historia ya soka.
Katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza, Luis Suárez aliokoa mpira kwa mkono akiwa golini na Ghana wakapewa penalti ambayo ingeipeleka Afrika katika nusu fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, Asamoah Gyan alikosa penalti hiyo kabla Ghana kupoteza kwa mikwaju ya penalti. Tukio hilo limeendelea kuwa moja ya simulizi zenye maumivu makubwa katika historia ya soka Ghana na Afrika kwa ujumla.
HEKAHEKA ZILIVYOKUWA
Licha ya kupitia misukosuko mingi katika miaka ya hivi karibuni, Ghana imefanikiwa kufuzu Kombe la Dunia 2026. Walifanya vizuri kwenye mechi za kufuzu hasa dhidi ya Mali na Madagascar waliokuwa wapinzani wakuu katika Kundi I na kuonyesha kuwa bado wana uwezo mkubwa wa kushindana wakiwa na pointi 25 kileleni. Safari yao ya kufuzu haikuwa rahisi. Kulikuwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashabiki kutokana na matokeo yasiyoridhisha huku kushindwa kufuzu AFCON 2025 kukiongeza presha kubwa ndani ya nchi hiyo.
MWANZO MPYA BLACK STARS
Moja ya mabadiliko makubwa kuelekea Kombe la Dunia 2026 ni ujio wa kocha mpya Carlos Queiroz. Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa duniani amewahi kuzinoa timu za Ureno, Iran, Colombia na Misri.
Queiroz amepewa jukumu la kuijenga upya Ghana na kuirudisha kwenye ushindani mkubwa wa kimataifa. Ujio wake umeonekana kama mwanzo mpya baada ya miaka kadhaa ya kutokuwa na utulivu ndani ya timu hiyo.
Kocha huyo anajulikana kwa nidhamu kubwa ya kiufundi, uwezo wa kupanga safu ya ulinzi na uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa. Ghana inaamini maarifa yake yanaweza kusaidia timu hiyo kufanya vizuri Marekani.
Kocha Queiroz ni muumini wa mfumo wa 4-1-4-1, wakati wakiwa na kocha Addo, Ghana ilikuwa ikitumia zaidi mfumo wa 3-4-1-2 ambao unabadilika na kuwa 5-4-1 wanapocheza na timu zenye upinzani mkali.
UBORA WA GHANA
Licha ya changamoto mbalimbali, Ghana bado ina kundi la wachezaji wenye vipaji vikubwa wanaocheza katika ligi bora duniani.
Nahodha wa timu hiyo ni Jordan Ayew ameichezea Ghana kwa zaidi ya mechi 110 na ni mmoja wa wafungaji bora wa muda wote wa taifa hilo. Nyota mwingine na kiungo Mohammed Kudus anayekipiga Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu England kwa sasa ni majeruhi kuna shaka ya kuwa sehemu ya kikosi hicho. Mbali na Kudus, pia wapo Thomas Partey (Villarreal), Inaki Williams (Athletic Bilbao), Antoine Semenyo (Manchester City), Kamaldeen Sulemana (Atalanta).
TATIZO LA GHANA
Pamoja na ubora wao, Ghana ina changamoto kadhaa kuelekea Kombe la Dunia. Tatizo kubwa limekuwa kutokuwa na muendelezo mzuri wa matokeo pamoja na migogoro ya ndani ya soka lao.
Katika miaka ya nyuma, Ghana imewahi kukumbwa na migomo ya wachezaji, migogoro ya posho, lawama dhidi ya viongozi wa shirikisho na matatizo ya kiutawala. Baadhi ya matatizo hayo yaliwahi kuharibu ushiriki wao katika Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Pia safu yao ya ulinzi imekuwa ikiruhusu mabao mengi katika mechi muhimu. Katika mechi za kirafiki za hivi karibuni, Ghana ilifungwa jumla ya mabao saba dhidi ya Austria (5-0) na Ujerumani (2-1), jambo lililoibua maswali kuhusu uimara wao kabla ya Kombe la Dunia.
UTAMADUNI WA BLACK STARS
Ghana ni moja ya nchi zenye mashabiki wa soka wenye mapenzi makubwa. Mechi zao nyingi hujazwa na maelfu ya mashabiki wanaoimba, kucheza na kuipa timu nguvu kama anavyopaswa kufanya mchezaji wa 12. Utamaduni wa Black Stars umejengwa katika muziki, dansi na uzalendo kwa taifa hilo. Nyimbo za kuhamasisha timu hiyo zimekuwa maarufu kila wanapokwenda katika mashindano makubwa.
Katika Kombe la Dunia 2010, dunia ilishuhudia shangwe za mashabiki wa Ghana pamoja na dansi maarufu zilizokuwa zikichezwa na wachezaji baada ya kufunga mabao.
REKODI ZA KIBABE
Katika historia ya Ghana, Andre Ayew ndiye mchezaji aliyeichezea timu hiyo mechi nyingi 120. Mfungaji bora wa muda wote ni Asamoah Gyan aliyefunga mabao 51. Gyan pia ndiye mchezaji wa Afrika mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia akiwa na mabao sita.
Majina mengine makubwa yaliyowahi kung’ara Ghana ni pamoja na Abedi Pele, Tony Yeboah, Michael Essien, Sulley Muntari na Stephen Appiah.