TIMU ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ leo itakuwa na kibarua cha pili kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON U-17) dhidi ya Angola mchezo wa Kundi C wa kufuzu Kombe la Dunia la Vijana.
Mechi hiyo itapigwa saa 12 kwa saa za Afrika Mashabiki katika Uwanja wa Mohammed VI Football Academy Pitch 11, Morocco yanapofanyika mashindano hayo yaliyoanza Mei 13 yakimalizika Juni 2.
Serengeti Boys inaingia uwanjani ikiwa na morali kubwa baada ya kuanza kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Msumbiji, huku Angola ikisaka ushindi wa kwanza baada ya kutoka suluhu dhidi ya Mali katika mchezo wa ufunguzi.
Ushindi wa Tanzania dhidi ya Msumbiji uliiweka kileleni mwa kundi na kuongeza tumaini la kufuzu mtoano kwa mara ya kwanza katika historia ya ushiriki AFCON U-17.
Hata hivyo, mbele kuna Angola ambayo ni miongoni mwa timu zenye ushindani mkubwa licha ya kutoka suluhu na Mali.
Ili kusaka ushindi mwingine Tanzania inapaswa kuwachunga baadhi ya nyota wa Angola ili wasilete madhara.
Angola inawategemea kiungo Costantino Chianica anayesaidia kucheza kwa uwiano wa kushambulia na kulinda pamoja na mshambuliaji Jairo Muanha.
Tanzania inashiriki AFCON U-17 kwa mara ya nne baada ya kushiriki pia mwaka 2017, 2019 na 2025, lakini mara zote ilishindwa kuvuka hatua ya makundi.
Mwanzo mzuri wa safari ya mwaka huu umeanza kuibua matumaini mapya kwa mashabiki wa soka nchini kuwa kizazi hiki kinaweza kuweka historia mpya kwenye ramani ya soka la vijana Afrika.
Kocha wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu alisema: “Maandalizi yamekamilika na kile ambacho nimewaelekeza wachezaji naamini wataenda kufanyia kazi kwenye mechi hiyo.”