Habari za michezo
POINTI MBILI TU YANGA WASISITIZA SIMBA HAWAWATISHI
Vardo
May 18, 2026
10:01 am
UONGOZI wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, umeweka wazi kuwa haupo kwenye presha yoyote licha ya tofauti ndogo ya alama mbili dhidi ya watani zao Simba katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu huu.
Kwa sasa Yanga wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 54, huku Simba wakifuatia nafasi ya pili na alama 52. Timu zote zimebakiza michezo nane ambayo inaweza kubadili kabisa taswira ya mbio za ubingwa huo zinazozidi kupamba moto kila siku.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, msemaji wa Yanga, Ali Kamwe amesema tofauti hiyo ya pointi inaonesha wazi jinsi ushindani wa ligi ulivyoongezeka kwa kiasi kikubwa msimu huu, tofauti na ilivyokuwa katika misimu iliyopita.
Kamwe amesema kuwa Yanga bado ipo kwenye mstari sahihi wa malengo waliyojiwekea tangu mwanzo wa msimu, jambo ambalo linawapa utulivu mkubwa kuelekea hatua za mwisho za mashindano yote wanayoshiriki.
“Hatuna presha kwa sababu bado tupo ndani ya malengo yetu. Tupo hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB na pia tunaongoza Ligi Kuu, hivyo tunaendelea kupambana kuhakikisha tunatimiza malengo yetu,” amesema Kamwe.
Ameikumbushia kauli yake ya awali kuhusu kuongezeka kwa ushindani wa ligi, akisema baadhi ya watu hawakuamini aliposema timu nyingi zimeimarika, lakini matokeo ya hivi karibuni yameanza kuthibitisha hilo baada ya Yanga kupoteza mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na kuzua mijadala mikubwa kwa mashabiki na wadau wa soka.
Kamwe amesisitiza kuwa Yanga haipewi nguvu na maneno ya nje wala presha kutoka kwa wapinzani wao, badala yake wanaendelea kuzingatia mipango yao ya ndani wakiamini bado wana nafasi kubwa ya kutetea taji lao la ligi msimu huu.