Habari za michezo

MZAMIRU NA CHAMOU WALIPOIKOSEKANA, SIMBA WAKAFANYA WANAVYOTAKA

Vardo May 18, 2026 9:56 am

KOCHA Mkuu wa TRA United, Etienne Ndayiragije, amesema kukosekana kwa nyota wake wawili, Mzamiru Yassin na Chamou Karaboue kuliiathiri kwa kiasi kikubwa timu hiyo katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba SC.

TRA United jana iliaga rasmi mashindano hayo baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Simba kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, huku wekundu hao wa Msimbazi wakitinga hatua ya nusu fainali kwa kishindo.

Ndayiragije alieleza kuwa kikosi chake kilikosa nguvu na uzoefu wa wachezaji hao wawili ambao kwa sasa wanaitumikia TRA kwa mkopo wakitokea Simba. Kwa mujibu wa makubaliano, nyota hao huwa hawaruhusiwi kucheza wanapokutana na klabu yao ya mama.

Kocha huyo amesema kuwa pengo la Mzamiru na Chamou lilionekana wazi ndani ya mchezo huo kutokana na ubora wao na mchango mkubwa waliokuwa wakiutoa katika kikosi chake msimu huu.

“Nina kikosi finyu sana, kuwakosa Mzamiru na Chamou kunaacha pengo kubwa sana. Wachezaji wangu wanacheza mechi nyingi pamoja na safari nyingi, lakini Simba wametuachia kiwango fulani cha utimamu wa mwili,” amesema Ndayiragije.

Pamoja na kipigo hicho kizito, kocha huyo amesema amepata mambo mengi ya kujifunza kupitia mchezo huo, huku akiahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi kabla ya kurejea kwenye mapambano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ndayiragije ameipongeza Simba kwa kiwango bora walichoonyesha na kusema walistahili ushindi huo kutokana na ubora wao pamoja na mipango mizuri ya benchi la ufundi.

“Ni ubora wao, tunapaswa kuheshimu ubora na mipango ya mwalimu wao. Mimi nimejifunza mengi kupitia mchezo huu na sasa naelekeza nguvu zote kwenye ligi,” amesema kocha huyo.

BARKER AIGEUZA SIMBA JESHI LA KIVITA, KILA MCHEZAJI TISHIO POINTI MBILI TU YANGA WASISITIZA SIMBA HAWAWATISHI