Habari za michezo
BARKER AIGEUZA SIMBA JESHI LA KIVITA, KILA MCHEZAJI TISHIO
Vardo
May 18, 2026
9:50 am
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kiwango kinachooneshwa na wachezaji wa kikosi hicho kwa sasa kinawapa utulivu mkubwa hata inapolazimu kufanya mabadiliko ya kikosi.
Ahmed amesema kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, amefanikiwa kujenga timu imara yenye ushindani mkubwa, ambapo kila mchezaji anayepata nafasi ana uwezo wa kufanya vizuri bila kujali ukubwa wa jina lake ndani ya kikosi hicho.
Ameeleza kuwa kutokuwepo kwa baadhi ya nyota hakujawa tatizo kwa Simba, akitolea mfano wa beki Shomari Kapombe ambaye amekosekana katika mechi tatu zilizopita lakini nafasi yake imezibwa vizuri na David Kameta ‘Duchu’.
“Hii ni mechi ya tatu Shomari Kapombe hayupo, lakini hakuna wasiwasi wowote. Anayepewa nafasi yake, David Kameta Duchu, anafanya kazi nzuri na hata ameweza kuwa mchezaji bora katika mechi ngumu kama hizi,” amesema Ahmed Ally.
Ahmed amesema Simba inaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda na sasa macho yao yote yameelekezwa katika kutimiza malengo ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu.
Akizungumzia kiwango cha kiungo mshambuliaji Clatous Chama, Ahmed amesema hakuna mchezaji anayeweza kumzuia nyota huyo kutimiza majukumu yake uwanjani kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza kwa utulivu, kufunga mabao na kutoa pasi za mwisho.
“Hakuna mchezaji ambaye anaweza kumzuia Clatous Chama asitimize majukumu yake uwanjani. Katika mechi ya jana alifanya kazi kubwa kabla ya kocha Barker kumpumzisha kwa ajili ymaandalizi ya mechi dhidi ya Coastal Union.Chama ana akili kubwa ya mpira, utulivu na uwezo mkubwa wa kubeba timu akiwa pamoja na wenzake,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa hata mchezaji aliyeingia kuchukua nafasi ya Chama aliweza kuonesha kiwango kizuri, jambo ambalo linaonesha wazi kuwa Simba ya sasa haitegemei mchezaji mmoja pekee, kwani yeyote anayepata nafasi ana uwezo wa kuisaidia timu kufanya vizuri.