Habari za michezo
TUNISIA WATAVUNJA MWIKO KOMBE LA DUNIA
Vardo
May 18, 2026
9:45 am
TUNIS, TUNISIA: KUNA timu ukizitazama unaweza usisikie kelele, mastaa wa gharama kubwa au presha kutoka kwa mashabiki wao, lakini katika mashindano makubwa zinageuka kuwa tishio miongoni mwao ni Tunisia.
Kwa miaka mingi, Tunisia ‘Tai wa Carthage’ wamekuwa wakijijengea heshima kupitia uimara wa safu ya ulinzi pamoja na uwezo wao wa kucheza mechi kubwa bila hofu yoyote.
Mara nyingi hawapewi nafasi, lakini kila kizazi wameendelea kubaki sehemu ya mataifa bora zaidi Afrika.
Wakiwa wamefuzu Kombe la Dunia mara saba na kushiriki AFCON mara 22, Tunisia ni moja ya timu zenye mwendelezo mkubwa zaidi katika soka la Afrika.
Rekodi yao ya kufuzu AFCON mara 17 mfululizo kuanzia 1994 mpaka 2025 imeendelea kuonyesha namna walivyobaki kwenye ushindani kwa muda mrefu kuliko mataifa mengi ya bara hili.
Safari yao Kombe la Dunia 2026 imeibua matumaini mapya kwa mashabiki wao. Baada ya miaka mingi ya kuishia hatua ya makundi, sasa wanaamini kizazi hiki kinaweza kuandika historia mpya kwa taifa lao kufuzu kwa hatua ya pili ya mashindano hayo makubwa zaidi duniani.
HISTORIA YAO
Soka lilianza kupata umaarufu Tunisia mwanzoni mwa karne ya 20 kipindi taifa hilo likiwa chini ya ukoloni wa Ufaransa. Kabla ya kupata uhuru 1956, tayari kulikuwa na timu isiyo rasmi iliyoundwa na wachezaji bora kutoka ligi ya Tunisia.
Mwaka 1928 waliucheza mchezo wao wa kwanza dhidi ya timu B ya Ufaransa, lakini wakapokea kipigo kizito cha mabao 8-2.
Katika miaka hiyo walikuwa wakicheza zaidi dhidi ya timu za Kifaransa pamoja na vikosi vya kijeshi.
Baada ya kupata uhuru Machi 20, 1956, Tunisia ilianza kujenga rasmi mfumo wake wa soka. Shirikisho lao la soka lilianzishwa mwaka 1957, huku taifa hilo likianza kushiriki mashindano ya kimataifa kama nchi huru.
Mchezo wao wa kwanza rasmi ulikuwa dhidi ya Libya katika Arab Games na walishinda mabao 4-3. Tangu hapo, soka likageuka kuwa sehemu muhimu ya utambulisho wa taifa hilo.
WALIVYOIBADILISHA AFRIKA 1978
Kwa Waafrika wengi, Tunisia itabaki milele kwenye historia ya Kombe la Dunia kutokana na walichokifanya mwaka 1978, Argentina.
Walipofuzu mashindano hayo, wengi hawakuwa wanawapa nafasi kubwa. Kipindi hicho timu za Afrika zilikuwa hazipewi heshima kwenye soka la dunia na mataifa mengi ya Ulaya yaliamini bara hili haliwezi kushindana kwa kiwango cha juu, lakini Tunisia walibadilisha simulizi hiyo.
Katika mchezo wao wa kwanza waliifunga Mexico mabao 3-1 na kuwa taifa la kwanza kutoka Afrika pamoja na nchi ya kwanza ya Kiarabu kushinda mechi ya Kombe la Dunia.
Ushindi huo uliishtua dunia na kuifanya FIFA kuanza kuangalia tofauti uwezo wa mataifa ya Afrika. Kwa wengi, hiyo ilikuwa moja ya hatua zilizofungua milango ya heshima kwa soka la Afrika kwenye mashindano makubwa duniani.
Ingawa hawakuvuka hatua ya makundi, Tunisia waliondoka Argentina wakiwa wameandika historia ambayo inatajwa mpaka leo.
MABINGWA WA AFRIKA
Kwa miaka mingi Tunisia walikuwa wakijulikana kama taifa lenye timu nzuri, lakini iliyokuwa inakosa bahati.
Walifika hatua za mwisho mara kadhaa, lakini walikuwa wanashindwa kumalizia kazi. Ndoto yao kubwa ilitimia 2004 walipoandaa AFCON kwenye ardhi yao.
Mashabiki wao waliinua taifa lote huku viwanja vikijaa kila mchezo. Chini ya Roger Lemerre, Tunisia ilijenga timu yenye utulivu pamoja na uwezo wa kucheza kwa kujiamini mbele ya mashabiki wao.
Waliondoa Senegal robo fainali kabla ya kuifunga Nigeria kwenye nusu fainali. Katika fainali dhidi ya Morocco, Mehdi Nafti waliinua matumaini mapema kabla ya Francileudo Santos kufunga bao lililowapa ushindi wa mabao 2-1.
Usiku huo uliifanya Tunisia kutwaa AFCON yao ya kwanza katika historia huku Roger Lemerre akiandika rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kushinda Euro na AFCON.
Mafanikio hayo yaliifanya Tunisia kuwa moja ya mataifa yaliyokuwa yanaogopwa zaidi Afrika kipindi hicho.
WALIVYOPOROMOKA
Baada ya mafanikio ya 2004, Tunisia iliendelea kushiriki mashindano makubwa lakini ilianza kupoteza ule ubora wa awali.
Walifuzu Kombe la Dunia 2006, lakini walitolewa hatua ya makundi baada ya kukutana na Hispania, Ukraine na Saudi Arabia. Hata hivyo walionesha ushindani mkubwa licha ya kushindwa kusonga mbele.
Miaka iliyofuata ikawa ngumu zaidi. Walikosa Kombe la Dunia 2010 huku wakibadilisha makocha mara kwa mara na kupoteza mwelekeo zaidi.
Matokeo mabaya yaliwafanya washuke mpaka nafasi ya 65 kwenye viwango vya FIFA 2010 ambayo ndiyo nafasi yao mbaya zaidi kuwahi kufikiwa.
Lakini hata walipokuwa wanayumba, Tunisia iliendelea kubaki moja ya timu ngumu zaidi kucheza nayo Afrika kutokana na nidhamu yao ya kiuchezaji.
WALIVYOAMKA TENA
Mwaka 2018 Tunisia waliinuka tena baada ya kufuzu Kombe la Dunia Russia. Kabla ya mashindano hayo walitoa sare dhidi ya Ureno na Uturuki kwenye mechi za kirafiki huku wakionesha kiwango kizuri dhidi ya Hispania.
Matokeo hayo yaliifanya Tunisia kupanda mpaka nafasi ya 14 kwenye viwango vya FIFA, nafasi bora zaidi kuwahi kufikiwa katika historia yao. Ingawa walitolewa tena hatua ya makundi Russia, waliifunga Panama mabao 2-1 na kuondoka na heshima.
Kwenye AFCON 2019 waliendelea kuonyesha uimara wao baada ya kufika nusu fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15.
Waliondoa Ghana na kuifunga Madagascar mabao 3-0, kabla ya kuishia nusu fainali mbele ya Senegal.
Mashabiki wengi waliamini Tunisia ilikuwa inaanza kurudi kwenye ubora wake wa zamani.
WALIVYOISHTUA DUNIA QATAR
Katika Kombe la Dunia 2022, Qatar, Tunisia waliandika historia nyingine wakiwa kundi moja na mabingwa wa dunia Ufaransa, Denmark pamoja na Australia. Wengi walidhani wangetolewa kirahisi, lakini Tunisia walipambana kiume.
Baada ya sare dhidi ya Denmark na kupoteza kwa Australia, waliingia mchezo wa mwisho dhidi ya Ufaransa wakiwa hawapewi nafasi. Lakini kupitia bao la Wahbi Khazri, Tunisia waliifunga Ufaransa bao 1-0 na kuandika moja ya ushindi mkubwa zaidi katika historia yao.
Ingawa walishindwa kuvuka hatua ya makundi kutokana na ushindi wa Australia dhidi ya Denmark, waliionyesha dunia bado wana uwezo wa kusimama mbele ya mataifa makubwa.
KIZAZI CHA SASA
Kwa sasa Tunisia ina kizazi kipya ambacho kinaonekana kuwa na mchanganyiko mzuri wa uzoefu na vijana wenye njaa ya mafanikio.
Youssef Msakni ambaye anaichezea Esperance ya nchini kwao bado anaendelea kuwa moyo wa timu kutokana na uzoefu wake mkubwa pamoja na uwezo wake wa kubeba presha ya mechi kubwa.
Kiungo Hannibal Mejbri ambaye anaichezea Burnley anaonekana kuwa moja ya vipaji vikubwa zaidi kuwahi kutoka Tunisia katika miaka ya karibuni kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi pamoja na kuchezesha timu, ikumbukwe kuwa huyu alikuwa Manchester United.
WALIVYOFUZU
Safari yao ya kuelekea Kombe la Dunia 2026 ilikuwa ya kipekee.
Baada ya kupitia misukosuko ya kisiasa ndani ya shirikisho lao pamoja na mabadiliko ya makocha, wengi hawakuwa na uhakika kama Tunisia ingeweza kurejea kwenye ubora wake.
Lakini chini ya Sami Trabelsi, Tai wa Carthage waliinuka tena.
Oktoba 13, 2025 waliandika historia mpya baada ya kuwa timu ya kwanza kufuzu Kombe la Dunia bila kuruhusu bao lolote katika mechi za kufuzu.
Rekodi hiyo ilionesha namna Tunisia ilivyokuwa imara kiulinzi pamoja na nidhamu kubwa waliyoonyesha katika harakati zao za kufuzu wakiwa kundi H, walimaliza vinara wakiwa na pointi 28.
WANACHOKITAFUTA
Kwa miaka mingi Tunisia imekuwa ikipewa heshima Afrika kutokana na muendelezo wao wa mafanikio.
Wamewahi kuwa mabingwa wa Afrika, wamewahi kuandika historia Kombe la Dunia na wameendelea kubaki kwenye ushindani mkubwa kwa muda mrefu.
Lakini bado kuna jambo moja kubwa ambalo hawajawahi kulifanya. Hawajawahi kuvuka hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Hiyo ndiyo ndoto kubwa ya Tai wa Carthage kuelekea Marekani, Canada na Mexico 2026.
Na kwa namna kizazi hiki kilivyojengwa, nidhamu waliyonayo pamoja na uzoefu wao kwenye mashindano makubwa, Tunisia ipo Kundi F pamoja na Sweden, Japan na Uholanzi, inaamini safari hii inaweza kuwa tofauti.