Habari za michezo

SIMBA YASUBIRI KOSA LA YANGA KUTWAA USUKANI

Vardo May 20, 2026 9:09 am

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema bado wanaamini katika mbio za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akisisitiza kuwa nafasi yao ya kupambana bado ipo wazi huku wakiahidi kupigania ushindi katika kila mchezo uliosalia.

Ahmed amesema matokeo ya hivi karibuni ya wapinzani wao wakubwa, Yanga SC, yameonyesha kuwa chochote kinaweza kutokea katika hatua hizi za mwisho za ligi, jambo ambalo limeongeza morali kwa Simba kuendelea kusaka pointi muhimu.

Ameeleza kuwa Yanga, ambao walikuwa mbele kwa tofauti ya alama tano, tayari wameanza kupoteza pointi baada ya kutoka sare dhidi ya Dodoma Jiji FC, hali ambayo imefufua matumaini kwa Simba katika mbio za ubingwa.

“Alama mbili hata tusipozifikia moja kwa moja, lakini zinatupa nguvu ya kuendelea kuwafukuzia. Tofauti hiyo ni mechi moja tu, anaweza kutoka sare au kupoteza na sisi tukajikuta tupo kileleni,” amesema Ahmed.

Ahmed amesema jambo muhimu kwa sasa si kuangalia matokeo ya wapinzani pekee, bali kuhakikisha Simba inashinda michezo yake yote iliyobaki ili kuendelea kuweka presha kubwa katika mbio za ubingwa hadi mwisho wa msimu.

“Si rahisi kutegemea wapinzani waendelee kudondosha pointi kila wakati. Kikubwa ni sisi kushinda kila mechi iliyopo mbele yetu, halafu ligi ikimalizika tutajua nani amevuna nini,” amesema.

Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Coastal Union, Ahmed amesema Simba imewasili Tanga ikiwa na dhamira ya kusaka ushindi licha ya kutambua ugumu wa mchezo huo kutokana na ubora wa wapinzani wao wanapokuwa nyumbani.

“Tumejiandaa vizuri kwa mchezo huu. Tunajua Coastal Union ni timu ngumu hasa wanapocheza nyumbani, lakini sisi tumekuja kupambana na kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu,” amesema Ahmed huku akiongeza kuwa kikosi walichosafiri nacho kiko tayari kwa mchezo huo muhimu.

Kikosi cha Simba kipo Tanga kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Alhamisi 21, 2026, Uwanja wa Mkwakwani.

MBONGO NA KIBARUA CHA KUIBEBA QUATAR KOMBE LA DUNIA TANZANIA NA ENGLAND KUSHIRIKIANA KUKUZA MICHEZO