Habari za michezo

TANZANIA NA ENGLAND KUSHIRIKIANA KUKUZA MICHEZO

Vardo May 20, 2026 9:17 am

NGULI wa soka duniani, Rio Ferdinand, amekabidhiwa jezi maalumu ya timu ya Dar City katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa maendeleo ya soka kati ya Tanzania na Uingereza.

Hafla hiyo iliongozwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabeet.

Tukio hilo limeelezwa kuwa mwanzo wa ushirikiano mpana wenye lengo la kuinua michezo nchini kupitia uwekezaji, kubadilishana uzoefu na kuendeleza vipaji vya vijana. Rio Ferdinand, ambaye aliwahi kutamba akiwa beki wa klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya England, ameonesha kuvutiwa na juhudi zinazofanywa Tanzania kukuza sekta ya michezo.

Katika mazungumzo yao, Ferdinand na Thabeet walisisitiza umuhimu wa kutumia michezo kama daraja la maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia walieleza dhamira yao ya kushirikiana katika programu mbalimbali zitakazosaidia vijana kupata mafunzo bora, sambamba na matumizi ya teknolojia katika kuendeleza michezo ya kisasa.

Mbali na hilo, viongozi hao walizungumzia umuhimu wa kuanzisha kliniki za michezo, programu za kubadilishana uzoefu wa kimataifa pamoja na kujenga mifumo endelevu ya mafunzo kwa vijana wenye vipaji.

Lengo kubwa likiwa ni kutoa nafasi pana zaidi kwa vijana wa Kitanzania kuonesha uwezo wao katika majukwaa ya kimataifa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amepongeza hatua hiyo na kusema ni mwanzo mzuri wa kufungua milango ya maendeleo ya michezo nchini kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Amesema uwepo wa watu wenye ushawishi mkubwa katika michezo unaweza kuongeza hamasa na kuleta mabadiliko makubwa kwa vijana wa Tanzania.

Makonda ameeleza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazolenga kuboresha miundombinu ya michezo na kukuza vipaji vya vijana.

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo unaweza kuwa chanzo cha kuongeza fursa za ajira na maendeleo kwa vijana wanaojikita katika michezo mbalimbali

SIMBA YASUBIRI KOSA LA YANGA KUTWAA USUKANI SIMBA YATAWALA ARUSHA, REKODI NZURI YAZUA HOFU KWA COASTAL UNION