Habari za michezo

SIMBA YATAWALA ARUSHA, REKODI NZURI YAZUA HOFU KWA COASTAL UNION

Vardo May 20, 2026 9:21 am

MATARAJIO yamepanda kwa mashabiki wa Simba SC kufuatia taarifa ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Coastal Union kuchezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, hatua ambayo imezua matumaini makubwa ya ushindi kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi.

Wengi wa mashabiki hao wanaamini kuwa mazingira ya Arusha yanaweza kuwa chachu muhimu ya mafanikio kwa timu yao, hasa kutokana na historia nzuri ya matokeo ambayo Simba imekuwa ikiyapata inapocheza katika eneo hilo msimu huu.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ambaye amesema Arusha imeendelea kuwa sehemu yenye kumbukumbu nzuri kwa kikosi hicho kila kinapokwenda kucheza michezo ya mashindano mbalimbali.

Ahmed amesema Simba imekuwa ikionyesha kiwango bora katika mechi zake zilizopita zilizochezwa Arusha msimu huu, jambo ambalo limeongeza morali kwa wachezaji pamoja na mashabiki kuelekea pambano hilo muhimu dhidi ya Coastal Union.

Ameeleza kuwa katika michezo mitatu iliyopita ambayo Simba imecheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid msimu huu, timu hiyo imepata matokeo mazuri yaliyowajengea hali ya kujiamini, huku mazingira ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid yakionekana kuwa rafiki zaidi kwa kikosi hicho.

Mbali na rekodi za msimu huu, Ahmed amesema historia ya Simba dhidi ya Coastal Union jijini Arusha pia inaipa matumaini makubwa timu hiyo, kwani mara kadhaa wamekuwa wakipata ushindi wanapokutana na wapinzani hao kwenye dimba hilo.

Ameongeza kuwa Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na lengo moja tu la ushindi, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao katika safari hiyo ya kusaka tiketi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

TANZANIA NA ENGLAND KUSHIRIKIANA KUKUZA MICHEZO IBENGE AWANIA UKOCHA MALI, AZAM FC YATAZAMA MUSTAKABALI WAKE