Yanga SC

BAADA YA KUPITIA MAGUMU …, MWAMNYETO ARUDI NA JIPYA YANGA SC

Vardo May 20, 2026 9:40 am

NAHODHA wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto, ameweka wazi kuwa amerudi katika hali nzuri ya utimamu wa mwili na akili, akisisitiza kuwa sasa yupo tayari kupambana katika michezo iliyosalia ya Ligi Kuu.

Mwamnyeto amesema dhamira yake kubwa kwa sasa ni kuhakikisha Yanga SC inakusanya alama tatu katika kila mchezo uliobaki wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.

β€œNimerejea kikosini niko fiti kabisa. Kazi yangu ni kuhakikisha timu inapata ushindi katika kila mechi zilizobaki ili tuendelee kutetea ubingwa wetu,” amesema nahodha huyo.

Nahodha huyo hakuwamo kwenye kikosi kilichocheza mchezo wa robo fainali ya CRDB dhidi ya JKT Tanzania, kutokana na changamoto za kisaikolojia zilizomlazimu kuomba muda wa mapumziko.

Inaelezwa kuwa Mwamnyeto alipitia wakati mgumu baada ya kupokea ujumbe mbalimbali kutoka kwa baadhi ya mashabiki kufuatia tukio la kujifunga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji FC, hali iliyoathiri hali yake ya kiakili.

Kutokana na hali hiyo, uongozi pamoja na benchi la ufundi walimpa muda wa kupumzika ili kumsaidia kurejea katika utimamu wake wa kawaida kabla ya kurejea tena mazoezini.

Kwa sasa, nahodha huyo amerudi kambini akiwa na morali mpya na anatizamwa kama moja ya nguzo muhimu kwa Yanga SC katika safari ya kumaliza msimu kwa mafanikio makubwa.

KISA ‘UTAMU’ WA CHAMA….SIMBA WASHINDWA KUJISHIKILIA πŸ˜…πŸ˜…πŸ˜…….