Habari za michezo
TETEMEKO LAANZA TANZANIA CHAMA AMGEUZIA SIMBA NGUVU MPYA
Vardo
May 20, 2026
9:32 am
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameendelea kumtaja kiungo nyota Clatous Chama kama mchezaji wa kipekee mwenye hadhi ya juu, akisisitiza kuwa ubora wake umeandika historia ya aina yake katika soka la Tanzania tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo mwaka 1922.
Akizungumzia mchango wa kiungo huyo ndani ya kikosi cha Simba SC, Ahmed amesema hakuna mchezaji mwingine aliyewahi kufikia kiwango cha ubora na uthabiti kama wa Chama, jambo linaloifanya klabu hiyo kujivunia uwepo wake na kupata nguvu kubwa kila wanapojipanga kuwakabili wapinzani.
Ameeleza kuwa uwepo wa mchezaji wa aina ya Chama unabadilisha hata mtazamo wa mchezo kabla haujaanza, kwani huongeza imani na ari kwa wachezaji wenzake na benchi la ufundi, wakijua wana silaha ya kipekee uwanjani.
“Unapokuwa na mchezaji aina ya Chama inakupa nguvu unapoelekea kwenye mechi. Unatazama mpinzani, lakini pia unaangalia timu yako na uwezo wa wachezaji wako,” amesema Ahmed.
Amesisitiza kuwa Chama ni miongoni mwa wachezaji wanaoipa Simba SC faida ya kipekee kutokana na uwezo wake wa kuunganisha timu, kurahisisha uchezaji na kuchangia moja kwa moja kwenye matokeo chanya.
Ameongeza kuwa ubora wa kiungo huyo unaongezwa zaidi na uwepo wa wachezaji wengine wenye kiwango kikubwa ndani ya kikosi hicho, akiwataja Neo Maema, Libasse Gueye, Kante na Kagoma kama sehemu ya safu inayoifanya Simba kuwa timu yenye ushindani mkubwa.
Kwa mujibu wa Ahmed, mchanganyiko wa vipaji hivyo ndani ya kikosi cha Simba SC ndiyo unaowapa nguvu ya kupambana katika kila mchezo, huku akisisitiza kuwa lengo lao ni kuendelea kuboresha ubora wao na kuhakikisha klabu inafikia mafanikio makubwa zaidi katika michuano mbalimbali.