Habari za michezo
MBONGO NA KIBARUA CHA KUIBEBA QUATAR KOMBE LA DUNIA
Vardo
May 20, 2026
9:00 am
DOHA, QATAR: NYOTA mwenye asili ya Tanzania, Akram Afif anatarajiwa kwa mara nyingine tena kuiongoza Qatar katika fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kujumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 34 kilichotangazwa na kocha Julen Lopetegui.
Qatar ambao walikuwa wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022, wamerejea tena kwenye michuano hiyo baada ya kufuzu kupitia hatua ya nne ya mchujo wa Bara la Asia mwishoni mwa mwaka jana, 2025.
Afif ambaye ni mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa Qatar katika miaka ya hivi karibuni, anatajwa kuwa tegemeo kubwa la timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutengeneza nafasi na kufunga mabao. Nyota huyo wa Al Sadd SC anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji sambamba na mshambuliaji mwingine hatari, Almoez Ali wa Al Duhail SC.
Afif anahusishwa na Tanzania kupitia familia yake, hasa upande wa baba yake. Baba yake, Hassan Afif, alizaliwa Tanzania kabla ya kuhamia Mashariki ya Kati ambako aliendelea na maisha yake ya soka.
Kocha Lopetegui pia amewajumuisha wachezaji wawili wanaokwenda kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza ambao ni beki wa kushoto Ryan Al Ali wa Al Rayyan SC pamoja na beki wa kati Niall Mason wa Al Wakrah SC.
Mkongwe Sebastian Soria wa Qatar SC naye amejumuishwa kwenye kikosi hicho na ana nafasi ya kuweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kucheza Kombe la Dunia.
Soria mwenye miaka 42 anaweza kumpita Roger Milla wa Cameroon ambaye aliweka rekodi hiyo mwaka 1994 akiwa na miaka 42 na siku 39.
Katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2026, Qatar watakutana na Uswisi, Canada pamoja na Bosnia & Herzegovina.
CHIMBUKO LA QATAR (1940-1950)
Mpira wa miguu uliingia nchini Qatar katika kipindi kilichoenda sambamba na ugunduzi wa awali wa mafuta huko Dukhan mwaka 1940.
Kufikia 1948, timu mbalimbali zilikuwa zimeanzishwa na wafanyakazi wa mafuta kutoka mataifa tofauti kama India na nchi kadhaa za Kiarabu. Miongoni mwa timu za kwanza nchini humo kulikuwa na timu ya Northern Arab Region pamoja na timu iliyoundwa karibu na eneo la Al-Khatia mjini Dukhan.
Mashindano ya kwanza ya mpira yalikuwa Ezz Eddin Tournament’, yaliyoandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Qatar mwaka 1951. Mwishoni mwa miaka ya 1950, jina la mashindano hayo lilibadilishwa na kuitwa na Pukett Cupâ.
Kutokana na kuongezeka kwa mapenzi ya mpira wa miguu, Shirikisho la soka Qatar (QFA) ilianzishwa rasmi mwaka 1960 huku ikijiunga na FIFA mwaka 1963.
Katika kipindi hicho pia, Shirikisho la Soka la Bahrain lilianza kupanga kuanzishwa kwa mashindano ya kikanda ya nchi za Ghuba (GCC), ambapo viongozi wa Qatar walihusika kwa karibu katika maandalizi hayo. Mpango huo ulifanikiwa mwaka 1970 baada ya kuanzishwa rasmi kwa Kombe la Ghuba ya Kiarabu (Arabian Gulf Cup).
KUPANDA KWA SOKA QATAR
Qatar ilicheza mechi yake ya kwanza rasmi Machi 27, 1970, dhidi ya wenyeji Bahrain katika michuano ya Gulf Cup 1970, ambapo ilifungwa mabao 2-1. Bao pekee la Qatar lilifungwa na Mubarak Faraj.
Katika mashindano hayo, Qatar ilimaliza mkiani ikiwa na pointi moja pekee huku sare ya bao 1-1 dhidi ya Saudi Arabia ikiwa moja ya matokeo bora kwao. Mchezaji Khaled Ballan alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano.
Mwaka 1972, katika michuano mingine ya Gulf Cup, Qatar ilimaliza tena mkiani baada ya kupoteza mechi zote tatu. Hata hivyo, michuano ya 1974 ilikuwa mwanzo wa mafanikio kwa Qatar baada ya kupata ushindi wao wa kwanza wa kimataifa kwa kuifunga Oman mabao 4-0.
Baadaye, Qatar ilifungwa na Saudi Arabia katika hatua ya nusu fainali lakini ikaibuka na nafasi ya tatu baada ya kuifunga UAE kwa mikwaju ya penalti. Katika mashindano hayo, Mohammed Ghanim wa Qatar alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano.
Qatar pia ilishiriki hatua za kufuzu AFC Asian Cup mwaka 1976 lakini ilichemka. Licha ya kushindwa huko, Qatar iliendelea kuonyesha maendeleo kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Gulf Cup ya 1976 iliyofanyika nchini humo huku wachezaji kama Mansour Muftah, Khaled Ballan na Mohammed Ghanim wakianza kung’ara.
Timu ya taifa pia ilishiriki mechi za kufuzu Kombe la Dunia ya 1978. Qatar ilikuwa icheze dhidi ya UAE Machi 11, 1977 lakini kujitoa kwa UAE dakika za mwisho kulifanya mechi hiyo kuahirishwa. Hatimaye, Qatar ilicheza mechi yake ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia siku mbili baadaye na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bahrain mjini Doha.
ENZI YA DHAHABU
Qatar kwa kiasi kikubwa ilifikia kilele chake katika miaka ya 1990, ikifika hadi nafasi ya 53 kwenye viwango vya FIFA Agosti 1993.
Qatar ilianza mchakato wa kufuzu kwa Kombe la Dunia 1990 kwa kumaliza kileleni mwa kundi lake. Hata hivyo, haikusonga mbele baada ya kumaliza chini ya UAE na Korea Kusini katika hatua ya mwisho ya mchujo.
Katika Kombe la Ghuba la 1990, timu hiyo ilimaliza tena kama mshindi wa pili huku Kuwait ikishinda mechi mbili za mwisho za mashindano hayo.
Mwaka 1992, Qatar ilishinda Kombe la Ghuba ikiwa nyumbani kwa mara ya kwanza chini ya Sebastiao Lapola. Mubarak Mustafa alishinda tuzo ya mfungaji bora pamoja na mchezaji bora wa michuano hiyo. Pia walimaliza kama washindi wa pili katika Kombe la Ghuba la 1996.
Qatar ilifika hatua ya mwisho ya mchujo wa Kombe la Dunia 1998. Baada ya ushindi dhidi ya China na Iran, walicheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Saudi Arabia ambapo ushindi ungewapa nafasi ya kufuzu. Hata hivyo, walipoteza 1-0 na Saudi Arabia ikasonga mbele.
Kama wenyeji wa Kombe la Waarabu la 1998, walimaliza kama washindi wa pili nyuma ya Saudi Arabia.
MWENDO MDUNDO
Walifika robo fainali ya AFC Asian Cup mwaka 2000 licha ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi lao, lakini wakatolewa na China.
Walifika tena hatua ya mwisho ya mchujo mwaka 2001 lakini wakafungwa na China ya Bora Milutinovic iliyosonga mbele Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Kocha Mfaransa Philippe Troussier alichukua jukumu la ukocha baada ya Kombe la Dunia 2002 lakini hakufanikiwa katika Kombe la Asia la 2004 na mchujo wa Kombe la Dunia 2006.
Troussier alifukuzwa baada ya mechi za mchujo na chini ya kocha wa Bosnia, Dzemaludin Musovic, timu ilishinda Kombe la Ghuba 2004 pamoja na medali ya dhahabu ya Michezo ya Asia ya U-23 mwaka 2006.
Hata hivyo, Musovic alijiuzulu baada ya Qatar kupata pointi mbili tu katika mechi tatu za Kombe la Asia la 2007. Jukumu la ukocha kwa mchujo wa Kombe la Dunia 2010 lilienda kwa Jorge Fossati kutoka Uruguay lakini baadaye aliondoka.
KOMBE LA DUNIA
Licha ya mafanikio makubwa ya Qatar katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, Kombe la Dunia la 2022 ambalo lilifanyika nyumbani ilikuwa janga kwao.
Wakiwa wamepangwa katika Kundi A kama wenyeji, Qatar ilianza kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Ecuador katika mechi ya ufunguzi, ikifungwa mabao mawili katika kipindi cha kwanza na Enner Valencia na hivyo kuwa nchi ya kwanza mwenyeji kupoteza mechi yake ya ufunguzi.
Hali haikubadilika katika mechi ya pili dhidi ya Senegal ambapo walichapwa tena mabao 3-1 na kutolewa mapema, na kuwa nchi ya pili mwenyeji baada ya Afrika Kusini mwaka 2010 kuwa na rekodi hiyo.
Qatar pia ikawa timu ya kwanza mwenyeji kutolewa baada ya mechi mbili tu. Mohammed Muntari aliifungia Qatar bao lao la kwanza katika Kombe la Dunia kwenye mechi hiyo.
Baada ya kuondolewa kwao kuthibitika, mechi ya mwisho ilimalizika kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Uhoanzi na hivyo kuweka rekodi nyingine mbaya ya kuwa nchi ya kwanza mwenyeji kupoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi.
Miezi 14 baadaye, walijirekebisha katika 2023 AFC Asian Cup iliyofanyika pia nyumbani. Timu hiyo ilianza michuano kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Lebanon na ikaingia hatua ya 16 bora ikiwa kinara wa kundi bila kuruhusu bao lolote.
Walishinda Palestine mabao 2-1 na kisha Uzbekistan kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1 na kufika hatua ya nusu fainali.
Baada ya kuifunga Iran kwa ushindi mgumu wa 3-2 katika nusu fainali, walicheza fainali dhidi ya Jordan ambapo hat-trick ya penalti ya Akram Afif iliisaidia Qatar kushinda 3-1 na kutwaa taji lao la pili mfululizo la AFC Asian Cup.
Mwezi Oktoba 2025, Qatar ilijihakikishia kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kuifunga UAE mabao 2-1 katika Uwanja wa Jassim bin Hamad mjini Doha.
Matokeo hayo yaliashiria kufuzu kwao kwa mara ya kwanza kupitia mchakato wa kawaida wa mchujo wa AFC, tofauti na mwaka 2022 waliposhiriki kama wenyeji.