Habari za michezo

KIKOSI CHA MAYELE WAMEBAKI SITA YANGA

Vardo May 20, 2026 8:54 am

FISTON Kalala Mayele kama ulivyosikia amechaguliwa kuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa lake DR Congo kinachokwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Akiwa ni staa pekee anayecheza soka Afrika katika kikosi hicho, mshambuliaji huyo anayekwenda kuweka rekodi kubwa Yanga alikowahi kufanya kazi sasa wamebaki wenzake sita tu aliocheza nao.

Huu utaendelea kuwa utambulisho rasmi kwenye fainali hizo kwa Ligi Kuu Bara pamoja na kikosi cha Yanga kuwa na mchezaji ambaye aliwahi kucheza hapo na sasa anahudumu kwenye michuano mikubwa zaidi duniani.

Mayele kabla ya kutua Pyramids alikuwa akiichezea Yanga kwa mafanikio akiwapa ubingwa lakini akiwahi kuwa mfungaji bora na mchezaji bora wa ligi kabla ya kuuzwa kwa Waarabu hao kwa dau la Dola 500,000 Julai 2023, ambako alikwenda kuwapa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita. Mayele mchezo wake wa mwisho kuichezea Yanga ni Juni 9, 2023, mabingwa hao wakimalizia mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Prisons, wakishinda kwa mabao 2-0.

Kwenye  kikosi hicho cha Yanga kuna wachezaji wanane tu waliosalia hadi sasa na kati ya hao sita walianza kikosi cha kwanza wakiwemo kipa Djigui Diarra, mabeki Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdulla ‘Bacca’  ambao bado wanatamba kwenye first eleven ya kikosi hicho.

Wengine ni viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye hana nafasi ya kudumu na Mudathir Yahya anayeingia na kutoka kwenye kikosi huku kwenye benchi wakiwemo Kibwana Shomari hana nafasi ya uhakika  sasa na mshambuliaji Clement Mzize ambaye baadaye aliingia kipindi cha pili kwenye mchezo huo, lakini kwa sasa anasumbuliwa na majeraha.

Wachezaji ambao hawapo sasa na walianza kwenye mchezo huo ni beki Joyce Lomalisa, viungo Zawadi Mauya, Tuisila Kisinda,Kennedy Musonda wakati kwenye benchi wakiwemo Metacha Mnata, Stephanie Aziz KI, Yannick Bangala na David Bryson. Katika mechi hiyo, Mayele alifunga bao la kwanza dakika ya 34 akipokea asisti ya Sure Boy lakini mshambuliaji huyo akatengeneza bao la pili kwa kutoa pasi ya mwisho kwa kichwa likifungwa na Bangala aliyetokea benchi.

Wachezaji hao wote watamshuhudia mwenzao wa zamani akienda kuweka rekodi ya kucheza mashindano makubwa duniani akiwa staa pekee ambaye amecheza ligi ya Tanzania anayecheza fainali hizo za dunia kwa mara ya kwanza.

ANKO NZALA AFIXHUA ALIVYOMNASA MO DEWJI KUIGIZA NAE KOMEDI MBONGO NA KIBARUA CHA KUIBEBA QUATAR KOMBE LA DUNIA