Habari za michezo

ANKO NZALA AFIXHUA ALIVYOMNASA MO DEWJI KUIGIZA NAE KOMEDI

Vardo May 20, 2026 8:49 am

NYUMA ya pazia alichokifanya msanii wa vichekesho nchini, Aman Nzala ‘Anko Nzala’ kumshawishi mwekezaji na rais wa heshima wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ kufanya naye kazi, chanzo kimefichuliwa.

Hivi karibuni kipande kifupi cha video kilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kikimuonyesha Nzala akiwa na MO, ambapo sekunde chache baadaye simu yake iliita mlio kuwa jina la Rais wa Yanga Hersi Said, baadaye simu hiyo iliita tena na mlio kuwa jina la Mfadhili wa Yanga, Gharib Said (GSM), ambapo wakati simu hizo zinaita tajiri huyo alikuwa akigeuka kumtazama mwingizaji huyo kwa mshangao.

Soka la Bongo lilimtafuta Anko Nzala kujua aliwezaje kumshawishi Mo Dewji hadi akakubali kufanya naye komedi, amejibu malengo ya kwenda ofisini kwa tajiri huyo yalikuwa ni kikao cha kazi hasa masuala ya biashara.

“Baada ya kukamilisha mazungumzo yaliyonipeleka, nilipogundua Mo Dewji ni mtu safi na anatamani kuona vijana wanajikwamua kiuchumi, nikapata ujasiri wa kuliwasilisha wazo langu, alinishangaza zaidi alipokubali kirahisi na kuniambia kama unaona nikitokea katika video yako itakusaidia kukupa hatua zaidi haina shida. Napenda kukuona unafika levo za kimataifa kama anavyoona wachekeshaji wengine wakubwa nje ya nchi,” alisema Anko Nzala na kuongeza;

“Kabla sijawaza nitafanyaje alisema tunaweza kushuti, haikuchukua dakika nyingi kila kitu kukamilika na nilifanyia ofisini kwake, alinichonisisitiza ni ubunifu, uthubutu utakaonitofautisha na wengine na anatamani kuniona kimataifa.

“Nilipoiposti na kuiona inatrendi mitandaoni, akanipigia simu na kunipongeza akinitaka nijikite katika ubunifu wa kitu kipya kila siku pia nimepokea simu za vigogo wengine ambao siwezi kuwataja walioniambia naweza nikafanya vichekesho na mtu yeyote, kikubwa ni kuangalia ni kontenti ya aina gani.”

Anko Nzala anayemuita Mo Dewji baba akitoa sababu ni kutokana na kuishabikia na kuipenda Simba, alisema alipokea simu za wachezaji kutoka timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara ikiwemo wanaocheza Simba ambao ni Shomari Kapombe, Elie Mpanzu, Libasse Gueye, Ladack Chasambi na Neo Maema ambaye alisema kuna kazi anafanya naye anatarajia kuiachia hivi karibuni.

KOCHA COASTAL AKWEPA MTEGO WA CHAMA KIKOSI CHA MAYELE WAMEBAKI SITA YANGA