Habari za michezo

KOCHA COASTAL AKWEPA MTEGO WA CHAMA

Vardo May 20, 2026 8:45 am

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema mechi dhidi ya Simba ni wa malengo kwa timu hiyo, huku akitaja mkakati maalumu wa kumdhibiti, Clatous Chama ambaye amekuwa gumzo kwenye michezo minne iliyopita ya Ligi Kuu pamoja na ule wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA, juzi.

Mchezo huo wa Ligi Kuu unatarajia kupigwa Mei 21, Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga ukiwa wa raundi ya 24 kwa timu hizo na Simba ipo nafasi ya pili na pointi 52, huku Coastal Union ni ya 11 na pointi 25.

Utamu wa mchezo huo ni kutokana na ubora wa timu hizo ambazo kwa mechi za nyuma zimekuwa na matokeo mazuri ikiwamo kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (CRDB) na zinatarajia kukutana tena kusaka nafasi ya fainali ya michuano hiyo.

Katika mechi mbili za mwisho, Coastal Union imeshinda mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City kabla ya kuwatoa Singida Black Stars kwenye Shirikisho kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 mechi kumalizika kwa suluhu.

Kwa upande wa Simba haijapoteza mchezo wowote tangu Mei 3, 2026 ilipocheza dhidi ya watani zao Yanga iliyoisha kwa sare ya 2-2, kisha kushinda dhidi ya JKT Tanzania 1-0, Prisons 4-0, Mashujaa 3-0 na 4-0 dhidi ya TRA United kwenye  Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, nyota wa Simba Chama ameonekana kuwa mwiba mkali akifunga mechi tano mfululizo akianza dhidi ya Yanga hadi mchezo dhidi ya TRA United akiipa matokeo mazuri timu hiyo inayofukuzia ubingwa wa Ligi Kuu iliyoukosa misimu minne sasa.

Akizungumza na Soka la Bongo, Elias amekiri ugumu wa mchezo huo na utakuwa wa malengo kwa timu zote kutokana na mahitaji ya sasa kwa pande hizo ikiwemo kukwepa kushuka daraja na ubingwa ambao unawaniwa na Simba.

“Ni mchezo wa malengo, sisi hatuko sehemu nzuri hivyo tunahitaji pointi tatu ili zitupeleke juu, wakati huohuo Simba wapo katika mbio za ubingwa hivyo lazima tutumie akili, mbinu na mkakati maalumu.”

“Tutacheza na Simba na wala siyo Chama au mtu mmoja, tunajua ubora wake na tutaweka mkakati maalumu kwenye beki yetu kuhakikisha hawaruhusu mashambulizi yoyote, lakini Chama tunamfahamu ni mchezaji mzuri tutapambana kwa kila hali ili kuhakikisha haleti madhara kwetu,” alisema kocha huyo.

Timu hizo zimekuwa zikionyesha kiwango cha juu kila zinapokutana na msimu uliopita zilitoka sare ya mabao 2-2, matokeo ambayo yalififisha ubingwa wa Simba. Katika mchezo wa kwanza msimu huu Simba ilishinda mabao 2-0.

LIGI TENA LEO

Hata hivyo, kabla ya mchezo huo Ligi Kuu itaendelea leo kwa michezo mitatu ambapo TRA itavaana na Mtibwa, KMC ikicheza na Pamba huku mchezo wa mwisho kwa leo ukiwa kati ya Dodoma na Mashujaa.

KISA UBINGWA KAMA ARSENAL…MO DEWJI ATIA NDIMU MASTAA SIMBA…. ANKO NZALA AFIXHUA ALIVYOMNASA MO DEWJI KUIGIZA NAE KOMEDI