Simba SC
Simba SC

KISA UBINGWA KAMA ARSENAL…MO DEWJI ATIA NDIMU MASTAA SIMBA….

admin May 20, 2026 1:07 am

ENDAPO Simba itabeba mataji mawili yaliyobaki msimu huu lile la Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB, basi mastaa wa kikosi hicho watavuta mkwanja wa Sh1 bilioni.

Hiyo ni ahadi kutoka kwa mwekezaji na rais wa heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’, baada ya hivi karibuni kukutana na kufanya nao kikao, lengo likiwa ni kuongeza morali kuhakikisha uhaba wa mataji unakoma Msimbazi.

Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa mitandao ya kijamii, basi utakuwa umegundua kuwa tajiri huyo wa Simba alikuwa mjini wikiendi iliyopita, huku akifanya vikao viwili vizito akianza na mastaa wa kikosi hicho, kisha mabosi wa juu.

Kikao cha kwanza Mo alianza na mastaa wa klabu hiyo ambao wamebadilisha upepo msimu huu wakianza na rekodi ya kuwanyima Yanga pointi tatu katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara, na kupokonya ufalme wa Kombe la Muungano dakika za jioni.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zilisema kuwa, Mo alianza kwanza na wachezaji na kuwapongeza kwa juhudi kubwa ambazo wameendelea kuzionyesha hasa katika Ligi Kuu.

“Mo amewaahidi wachezaji dau nono kama watafanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi na Kombe la CRDB, licha ya juhudi ambazo wameendelea kuzionyesha, lakini huu ndio wakati sahihi wa kurudisha heshima ya Simba.

“Mo aliwaambia kabisa kwamba, Simba ni timu kubwa na inaweza kuchukua ushindi ambao wameukosa kwa muda mrefu, kwani msimu huu wamejizatiti vizuri hivyo ni kazi ya wachezaji tu kukamilisha majukumu yao,” kilisema chanzo.

Kikao hicho kiliibua morali kwa mastaa hao kwani baada ya hapo walikutana na TRA United kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la CRDB na kushinda kwa mabao 4-0. Sasa Simba imefuzu nusu fainali itakwenda kucheza dhidi ya Coastal Union, Juni 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

KIKAO CHA MABOSI

Mabosi wa klabu hiyo walikutana na Mo Dewji katika kikao hicho walizidi kupanga mipango ya kuendelea kuisuka Simba ya maziwa na asali, ili kurudisha zama za mafanikio.

Taarifa za ndani zilisema kuwa, Mo aliwaambia viongozi kwamba kama wachezaji watafanikiwa kuchukua ushindi wa Kombe la CRDB na ligi atatoa zaidi ya Sh1 bilioni ikiwa ni pongezi.

“Tajiri kaweka bilioni moja pembeni tayari kwa ajili ya Simba kama itashinda makombe yote mawili yaliyosalia na kama atafurahi zaidi basi anaweza kuongeza mzigo.

“Hii ni taarifa njema kwa viongozi kwani kazi yao kubwa ni kuwapa morali mastaa ili wasije wakafeli na mzigo ukapotelewa hewani,” kilisema chanzo hicho.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Simba kuweka mzigo mezani kama morali, kwani msimu huu katika michuano ya Kombe la Muungano mabosi wa klabu hiyo waliweka Sh300 milioni kama watafanikiwa kuichapa Yanga na mpango ukatimia.

Hivyo Simba inaweza ikawa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kama tu Yanga itapoteza mchezo mmoja au sare na wao kushinda mechi zote saba zilizosalia.

Kwa sasa msimamo wa ligi unaonyesha Simba ipo nafasi ya pili ikiwa imecheza mechi 23, ikishinda 15, sare saba na kupoteza mmoja, ikifikisha pointi 52 ikizidiwa mbili na Yanga.

Mara ya mwisho Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2020-2021, pia ilibeba Kombe la Shirikisho (FA). Baada ya hapo, Yanga imechukua makombe hayo mara nne mfululizo huku msimu huu ikionekana kukutana na upinzani mkali.

ULIKUWA NA MIAKA MINGAPI MARA YA MWISHO ARSENAL WAKIBEBA KOMBE LA EPL?