Habari za michezo

KILIO CHA MWAMNYETO CHAMFANYA MOALLIN KUFUNGUKA HADHARANI

Vardo May 21, 2026 10:37 pm

KOCHA wa Yanga, Abdihalim Moallin amemkingia kifua nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, kufuatia presha na lawama zinazoendelea kumkabili beki huyo katika hatua hizi za mwisho wa msimu.

Moallin amesema kila mmoja anatambua ubora, uzoefu na mchango mkubwa wa Mwamnyeto ndani ya Yanga pamoja na soka la Tanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa makosa anayokutana nayo ni sehemu ya kawaida katika maisha ya mwanadamu na mchezo wa mpira wa miguu.

Kocha huyo ameeleza kuwa hata wachezaji wakubwa duniani hukosea mara kwa mara, lakini kinachowatofautisha ni uwezo wao wa kurejea kwa nguvu zaidi na kuendelea kupambana uwanjani.

Amesema Mwamnyeto ameendelea kuonyesha moyo wa uongozi na uzoefu mkubwa ndani ya kikosi hicho licha ya changamoto zinazojitokeza.

Moallin ameweka wazi kuwa benchi la ufundi bado lina imani kubwa na beki huyo kutokana na mchango wake mkubwa tangu alipojiunga na Yanga, huku akiamini ataendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu hiyo.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo dhidi ya Singida Black Stars, kocha huyo amesema kikosi kinaendelea vizuri na kila mchezaji anaelewa umuhimu wa kupata matokeo chanya katika mechi hiyo.

Amesema wanaiheshimu Singida Black Stars kwa ubora wao, lakini malengo makubwa ya Yanga ni kuhakikisha wanapata ushindi na kuondoka na alama tatu muhimu katika mbio za mwisho wa msimu.

“Tunajua umuhimu wa mchezo huu na tunahitaji alama tatu. Kikosi kipo tayari kupambana,” amesema Moallin.

Mbali na hilo, kocha huyo pia amegusia changamoto ya timu kushindwa kutumia baadhi ya nafasi ilizokuwa ikizitengeneza katika michezo ya hivi karibuni, akieleza kuwa eneo hilo linaendelea kufanyiwa kazi mazoezini.

Ameongeza kuwa licha ya mapungufu hayo, anafurahishwa na uwezo wa timu kuendelea kutengeneza nafasi nyingi za mabao, jambo ambalo linaonyesha uimara wa safu yao ya ushambuliaji na mwendelezo mzuri wa kiwango cha kikosi hicho.

AL NASSR KUTANGAZWA UBINGWA WA SOUD PRO LIGI MBELE YA DAMAC SIMBA WAUA MZUKA WA COASTAL, YANGA ATELEZA KWENYE KILELE