Habari za michezo

SIMBA WAUA MZUKA WA COASTAL, YANGA ATELEZA KWENYE KILELE

Vardo May 21, 2026 10:45 pm

KIKOSI cha Simba SC kimefanikiwa kuuteka Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union.

Matokeo yaliyoifanya timu hiyo kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuishusha Yanga . hadi nafasi ya pili.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa huku Coastal Union wakionyesha dhamira ya kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani mbele ya mashabiki wao.

Wenyeji hao walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya nane kupitia kwa Maabad Maulid aliyetikisa nyavu na kuipa timu yake uongozi wa bao 1-0.

Bao hilo lilionekana kuwashtua Simba ambao waliinua kasi ya mashambulizi wakisaka kusawazisha mapema kabla presha haijaongezeka.

Simba walionekana kucheza kwa nidhamu kubwa katikati ya uwanja huku wakimtegemea kiungo wao mahiri, Clatous Chama kuongoza mashambulizi.

Jitihada hizo zilizaa matunda dakika ya 37 baada ya mshambuliaji Libasse Gueye kufunga bao la kusawazisha kwa kichwa, akimalizia pasi safi iliyotengenezwa na Chama. Bao hilo liliwarejesha Simba mchezoni na kuongeza morali kwa wachezaji wake.

Baada ya kusawazisha, Simba waliendelea kuutawala mchezo huku Coastal Union wakionekana kuyumba katika safu yao ya ulinzi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wageni hao.

Dakika ya 44 Simba walifanikiwa kupata bao la pili kupitia kiungo mshambuliaji Anicet Oura aliyemalizia vizuri mpira uliotokana na kazi nzuri ya Chama, na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa huku Coastal Union wakijaribu kurejea mchezoni, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Simba uliwafanya wenyeji hao kushindwa kupata bao la kusawazisha hadi dakika 90 zilipomalizika.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 55 na kupanda hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiishusha Yanga hadi nafasi ya pili yenye pointi 54. Tofauti hiyo ya alama moja pekee imeendelea kuongeza ushindani mkubwa katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu.

KILIO CHA MWAMNYETO CHAMFANYA MOALLIN KUFUNGUKA HADHARANI FOUNTAIN GATE YAIBANIA JKT TANZANIA