Yanga SC
HATUJAMALIZA KAZI, NZENGELI PRESHA YANGA MBIO ZA UBINGWA
Vardo
May 24, 2026
9:44 am
KIUNGO wa Yanga SC, Maxi Nzengeli amesema ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu bado ni mkubwa huku akisisitiza kuwa wao kama timu hawajafikia malengo yao licha ya kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi mbalimbali.
Nzengeli amesema moja ya mechi zilizokuwa ngumu kwao ni dhidi ya Simba SC iliyopigwa Zanzibar, akieleza kuwa mchezo huo ulihitaji nguvu kubwa kutokana na ushindani na presha iliyokuwepo uwanjani.
“Mechi ya Simba ile ya ligi kule Zanzibar ilikuwa ngumu sana, tulipambana kwa kiwango kikubwa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Nzengeli.
Kiungo huyo ameweka wazi kuwa bado Yanga ina kazi kubwa mbele yao kwani ligi bado haijaisha na kila timu inapambana kutimiza malengo yake.
Amesema ndani ya kikosi hicho nguvu kubwa kwa sasa imeelekezwa katika kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa ligi, huku wachezaji wakiahidi kuendelea kupambana katika kila mchezo uliobaki.
“Bado hatujafikia malengo kwa sababu mechi zinaendelea na ushindani ni mkubwa sana katika ligi. Malengo yetu makubwa ni kupata ubingwa, hivyo tunaendelea kupambana kuhakikisha tunafikia tunachokitaka,” amesema.
Kauli ya Nzengeli inakuja wakati Yanga ikiendelea kuwa kwenye mbio kali za ubingwa huku mashabiki wakitarajia kuona timu hiyo ikiendeleza ubora wake katika mechi zilizobaki za msimu huu.