Simba SC

SIMBA YAONGEZA KASI SOKONI, MSHABULIAJI AZAM AINGIA KWENYE ORODHA

Vardo May 24, 2026 9:53 am

KATIKA kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, uongozi wa Simba SC umeanza kuangalia kwa umakini safu ya wazawa, ambapo jina la mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Hamisi Suleiman ‘Sopu’, limeibuka kuwa kwenye rada za klabu hiyo.

Sopu, ambaye aliwahi kuitumikia Simba kabla ya kujiunga na Coastal Union na baadaye Azam FC kutokana na kiwango chake bora, sasa ameripotiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia macho ya mabosi wa Wekundu wa Msimbazi.

Imeelezwa kuwa mazungumzo ya awali kati ya pande mbili yanaendelea vizuri, huku kilichosalia kikiwa ni makubaliano ya mwisho kati ya klabu hizo ili kukamilisha na kutangaza rasmi dili hilo.

Nyota huyo ameendelea kuonyesha ubora wake msimu huu akiwa miongoni mwa washambuliaji wa ndani wanaofanya vizuri zaidi, akijulikana kwa uwezo wake wa kufunga mabao, kutengeneza nafasi na uchezaji wenye nguvu eneo la ushambuliaji.

Ubora huo umesababisha klabu kadhaa kumweka kwenye rada zao, lakini Simba inaonekana kuwa mbele zaidi katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa upande wake, Simba imeingia mapema sokoni ikiwa na dhamira ya kuimarisha kikosi chake kwa wachezaji wenye uwezo wa kuleta ushindani zaidi katika kila idara, ikiwa ni sehemu ya mipango ya msimu ujao.

Inaelezwa pia kuwa kocha wa Simba, Steve Barker, amesisitiza umuhimu wa kuwa na kikosi kipana na chenye ushindani mkubwa, hali ambayo imeifanya klabu hiyo kuanza mapema kupanga usajili wa wachezaji watakaoweza kuongeza nguvu na kuleta mabadiliko chanya ndani ya timu.

HATUJAMALIZA KAZI, NZENGELI PRESHA YANGA MBIO ZA UBINGWA NAMUNGO SI MCHEZO RAHISI, KAMWE AONYA KABLA YA MTANANGE