Yanga SC
NAMUNGO SI MCHEZO RAHISI, KAMWE AONYA KABLA YA MTANANGE
Vardo
May 24, 2026
9:56 am
OFISA Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, ameweka wazi kuwa mchezo wao dhidi ya Namungo FC ni kama “derby ndogo” kutokana na ushindani mkubwa unaowakutanisha kila mara wanapokutana uwanjani.
Kauli hiyo imekuja huku Yanga wakijiandaa kusaka alama tatu muhimu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga SC watawakaribisha Namungo FC katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, wakijua wazi kuwa haitakuwa kazi rahisi mbele ya wapinzani hao wanaojulikana kwa upinzani mkali.
Akizungumza kuelekea mchezo huo muhimu, Kamwe amesema Namungo ni miongoni mwa timu zinazoleta changamoto kubwa kila wanapokutana na Yanga, jambo linaloufanya mchezo huo kuwa mgumu na wenye ushindani wa hali ya juu.
Ameongeza kuwa licha ya ubora wa kikosi cha Yanga SC msimu huu, hawatodharau mchezo huo hata kidogo, kwani kila timu sasa inapambana kwa nguvu zote kuhakikisha inafikia malengo yake ya msimu.
Kamwe pia amesisitiza kuwa Yanga SC imebakiza mechi sita pekee za ligi, hivyo hakuna nafasi ya kuchagua mechi, kwani kila mchezo kwao ni fainali katika mbio za kutetea ubingwa.
Amesema dhamira ya klabu ni moja tu—kuhakikisha wanakusanya pointi tatu katika kila mchezo uliobaki, wakibaki makini hadi mwisho ili kufanikisha azma ya kubaki kileleni na kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.