Simba SC

SIMBA QUEENS WATINGA MLANGONI KWA UBINGWA BAADA YA KUWATESA WAPINZANI

Vardo May 24, 2026 9:39 am

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema ubora ulioonyeshwa na Simba Queens msimu huu umetokana na uwezo wao wa kuwazidi wapinzani wao wakubwa.

Amesema katika mechi za ana kwa ana, jambo lililoweka timu hiyo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL).

Ahmed amesema timu zilizokuwa zikipewa nafasi ya kutoa ushindani mkubwa kwa Simba Queens ni JKT Queens pamoja na Yanga Princess, lakini Simba Queens wameonyesha kiwango bora kwa kupata matokeo mazuri dhidi yao ndani na nje.

Amesema JKT Queens walionekana kuwa wapinzani wakuu katika mbio za ubingwa kutokana na ubora wao msimu huu, lakini Simba Queens waliweza kuwafunga katika mchezo mmoja na kutoka sare kwenye mwingine, hali iliyowapa faida kubwa kwenye msimamo wa ligi.

Ahmed ameongeza kuwa dhidi ya Yanga Princess, Simba Queens walionyesha tofauti kubwa ya kiwango baada ya kushinda michezo yote miwili ya ligi, jambo lililoendelea kuthibitisha uimara wa kikosi hicho msimu huu.

“Msimu huu tumemuacha mbali JKT Queens kwa sababu tumefanikiwa kuwafunga kwao na kutoka sare. Halafu mpinzani mwingine anayekuwa anatupa presha, Yanga Princess, tumemfunga nje ndani,” amesema Ahmed.

Amefafanua kuwa kukusanya alama sita dhidi ya Yanga Princess na nne dhidi ya JKT Queens ni ishara kuwa Simba Queens wamejitenga kwa kiwango kikubwa na wapinzani wao katika mbio za ubingwa.

“Ukifanikiwa kuchukua alama sita kwa Yanga Princess na nne kwa JKT Queens maana yake huyo mpinzani umemuacha mbali,” amesema.

Ahmed amesema hadi sasa Simba Queens wamecheza mechi 18 huku wakibakiwa na michezo minne kumaliza msimu, na tayari wamejenga tofauti ya pointi 10 dhidi ya wapinzani wao wa karibu kwenye msimamo wa ligi.

Kwa mujibu wa Ahmed, ushindi katika mchezo wao ujao utaifanya Simba Queens kutangaza rasmi ubingwa wa ligi bila kujali matokeo ya timu nyingine zilizobaki kwenye mbio hizo.

“Mchezo unaofuata tukishinda basi Simba tutakuwa mabingwa, bila kuangalia matokeo ya mechi zao. Hata tukifungwa mechi tatu za mwisho na wao wakashinda zote, bado Simba itakuwa bingwa kwa pointi,” amesema Ahmed.

YANGA YAMUWINDA BITEGEKO KIMYA KIMYA HATUJAMALIZA KAZI, NZENGELI PRESHA YANGA MBIO ZA UBINGWA