SIMBA YACHEZA MECHI 16 KWA SIKU 52, BARKER ATOBOA SIRI
KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amefunguka sababu za kumtumia Elie Mpanzu katika safu ya ushambuliaji mbele ya mshambuliaji wa asili, Selemani Mwalimu, huku akieleza pia namna ratiba ngumu ya mechi ilivyoanza kuwaathiri wachezaji wa kikosi hicho.
Barker amesema uamuzi wa kumchezesha Mpanzu kama mshambuliaji haukuwa wa kubahatisha, bali ulitokana na uwezo wa mchezaji huyo kucheza nafasi tofauti uwanjani.
Kocha huyo alieleza kuwa Mpanzu aliwahi kucheza nafasi ya ushambuliaji hapo awali, jambo lililompa imani ya kumtumia katika mchezo huo muhimu.
“Mpanzu aliwahi kucheza kama mshambuliaji hapo kabla, tunajua ana uwezo wa kucheza sehemu mbalimbali, hivyo kwenye mchezo huu tulihitaji kitu tofauti,” amesema Barker.
Kocha huyo amepongeza kiwango na moyo wa kupambana wa wachezaji wake, akisema licha ya uchovu mkubwa waliokuwa nao, bado wameendelea kujituma na kupigania matokeo katika kila mchezo wanaocheza.
Hata hivyo, Barker hakuficha hisia zake kuhusu ratiba ya mechi ambazo Simba imekuwa ikicheza katika kipindi kifupi.
Amesema msongamano huo wa michezo unawaumiza wachezaji kimwili na kuongeza hatari ya kupata majeraha.
Kwa mujibu wa Barker, Simba imelazimika kucheza mechi 16 ndani ya siku 52 pekee, hali aliyodai si ya haki kwa wachezaji kutokana na presha kubwa ya ushindani na muda mdogo wa kupumzika.
“Ni mechi ya 16 ndani ya siku 52… si haki kwa wachezaji,” amesema kocha huyo kwa msisitizo.
Barker amesema mapumziko ya kimataifa ya FIFA yanakuja kwa wakati muhimu kwa kikosi chake, kwani yatawapa nafasi wachezaji kupumzika, kurejesha nguvu na kujiandaa vizuri kuelekea michezo ya mwisho ya msimu.
Simba sasa itaingia kwenye mapumziko hayo ikiwa na matumaini ya kurejea kwa nguvu mpya katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu huu.