DE RUCK AMKUBALI WILLIAM, ASEMA NI STRAIKA HATARI SANA
BEKI wa Simba SC, Rushine De Reuck, amemwaga sifa nzito kwa mshambuliaji wa Yanga SC, William Edgar, akimtaja kuwa mmoja wa washambuliaji wenye hatari zaidi kuwahi kukutana nao tangu aanze kucheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
De Reuck amesema licha ya kucheza dhidi ya washambuliaji wengi wenye uwezo tofauti, Edgar ameonyesha kiwango cha kipekee kutokana na namna anavyobaki kuwa tishio muda wote wa mchezo.
Kwa mujibu wa beki huyo wa Simba, mshambuliaji huyo wa Yanga ni aina ya wachezaji wanaowalazimisha mabeki kuwa makini kwa dakika zote 90.
Amesisitiza kuwa hata pale Edgar anapokuwa hana mpira, bado anaendelea kutengeneza mazingira ya hatari kupitia movement zake, jambo ambalo huwapa kazi kubwa mabeki wanaomkabili.
Kauli hiyo imeonekana kuwa heshima kubwa kutoka kwa mmoja wa mabeki tegemeo wa Simba kuelekea straika huyo wa Yanga anayeng’ara msimu huu.
Mbali na kumzungumzia mshambuliaji huyo wa Yanga, De Reuck pia ameonyesha kujiamini kuelekea mchezo wa Simba dhidi ya Dodoma Jiji FC katika Ligi Kuu.
Beki huyo amesema anaamini wekundu wa Msimbazi wataendelea kufanya vizuri katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.
Kauli za De Reuck zimeongeza hamasa mpya katika ushindani wa Simba na Yanga ambao unaendelea kupamba moto kadri msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara unavyozidi kuelekea tamati.