Kaizer Chiefs

KAZE, BEN YOUSSEF WAAGWA KAIZER CHIEFS

Vardo May 26, 2026 9:57 pm

KLABU ya Kaizer Chiefs, imethibitisha kuondoka kwa makocha Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze baada ya mikataba yao kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2025-2026.

Wawili hao awali waliteuliwa kuwa sehemu ya benchi la ufundi la kocha Nasreddine Nabi kabla ya Mtunisia huyo kuondoka katikati ya msimu. Pia wote wamewahi kufindisha Yanga SC.

Baada ya kuondoka kwa Nabi, Ben Youssef na Kaze walichukua jukumu la kuinoa timu hiyo kwa muda hadi mwisho wa msimu uliomalizika Mei 23, 2026.

Amakhosi walikuwa na msimu mwingine wa kusikitisha baada ya kumaliza bila kutwaa taji lolote, huku wakishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ikikusanya pointi 54, nyuma ya mabingwa Orlando Pirates (pointi 69) na mabingwa wapya wa Afrika, Mamelodi Sundowns (pointi 68).

Hata hivyo, klabu hiyo yenye makazi yake Naturena, imefanikiwa kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Katika taarifa yake, Chiefs iliwashukuru makocha hao wanaoondoka kwa mchango wao kwa klabu hiyo.

“Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa makocha hawa kwa kujitolea na mchango wao kwa klabu na tunawatakia kila la heri katika maisha yao yajayo,” imesema taarifa ya klabu hiyo.

Ben Youssef alijiunga na Amakhosi mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025, huku Kaze akiwasili Oktoba 2024.

Katika msimu wa 2025-2026, makocha hao waliiongoza Chiefs katika mechi 39 za mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Kombe la Shirikisho Afrika, Carling Knockout Cup na Nedbank Cup. Timu ilifanikiwa kushinda mechi 19, sare 11 na kupoteza 9.

NIGERIA KITEST MITAMBO DHIDI YA ZIMBABWE MECHI ZA KIRAFIKI RISASI YAANZA VIZURI LIGI YA KIKAPU SHINYANGA