Habari za michezo

MWAJANGA AIPA PRISONS POINTI TATU, PAMBA JIJI IKILOA KILUMBA

Vardo May 26, 2026 10:20 pm

BAO la dakika ya 90+4 la mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Oscar Mwajanga, limetosha kuipa timu hiyo ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Pamba Jiji, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa leo Mei 25, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute, Prisons ilianza kupata bao dakika ya 45 likifungwa na Haruna Chanongo, kisha Mkenya Mathew Momanyi akaisawazishia Pamba Jiji dakika ya 68 kisha akaongeza la pili dakika ya 71.

Hata hivyo, wakati Pamba Jiji ikifunga mabao hayo, Prisons ilijibu mapigo na kusawazisha dakika ya 78 kwa bao la penalti ya mshambuliaji, George Mpole aliyerejesha matumaini upya ya kikosi hicho cha maafande kinachopigania kutoshuka daraja.

Wakati mechi hiyo ikionekana inaisha sare ya mabao 2-2, Mwajanga aliyeingia dakika ya 80, akichukua nafasi ya Mpole akaifungia timu hiyo bao la tatu dakika ya 90+4, akimalizia mpira wa krosi ya Kelvin Sengati.

Ushindi kwa Prisons umefufua matumaini ya timu hiyo ya kupambania kubaki Ligi Kuu baada ya kutokuwa na mwenendo mzuri tangu msimu umeanza, ambapo kwa sasa imeshinda mechi tano, sare tano na kupoteza 15, ikishika nafasi ya 15 na pointi 20.

Pia, ushindi huo wa Prisons ni wa pili kwa Kocha Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ tangu alipojiunga nayo Februari 27, 2026, akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyeondoka Februari 25, 2026.

Otieno aliyejiunga na Prisons, Julai 24, 2025, kwa msimu wa 2025-2026 aliiongoza timu hiyo katika mechi 14 za Ligi Kuu, kati ya hizo alishinda tatu, sare tatu na kupoteza nane, ikifunga mabao manane na kuruhusu 16.

Katika mechi hizo 14, Otieno aliiacha Prisons ikiwa nafasi ya 14 na pointi 12, huku Mkenya huyo akizifundisha pia Gor Mahia FC, Sony Sugar, Posta Rangers na KCB FC zote za kwao Kenya na timu ya taifa ya Kenya maarufu ‘Harambee Stars’.

Tangu Februari 27, 2026, Nsajigwa amekiongoza kikosi hicho cha Prisons katika jumla ya mechi 11 za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo ameshinda mbili sawa na sare, akipoteza saba, huku timu ikifunga mabao saba na kuruhusu 20.

Kwa upande wa Pamba Jiji, katika mechi 25 ilizocheza msimu huu, imeshinda nane, sare tisa na kupoteza nane, huku ikifunga mabao 25 na kuruhusu 27, ikishika nafasi ya saba baada ya kukusanya pointi 33.

LEO NI WEWE AU NANI..?JANGWANI PESA ZIMEJAA SINGIDA YAICHELEWESHA KMC KUSHUKA IKIICHAPA MBEYA CITY